Dk Bashiru: Serikali ya 2010 ilikosa uhalali kisiasa

0
1142

Na Mwandishi Wetu – Morogoro

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, mwaka 2010 nchi ilipata Serikali ambayo haikuwa na uhalali wa kisiasa.

Dk. Bashiru aliyasema hayo jana mjini hapa, alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) lililofanyika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro.

Alisema Serikali hiyo ilipatikana kwa sababu zaidi ya asilimia 50 ya wapigakura waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza siku ya uchaguzi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Jakaya Kikwete alichanguliwa kuongoza Serikali kwa awamu ya pili, wapigakura waliojiandikisha walikuwa 20,137,303 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84.

Jana akizungumza mjini hapa, Dk. Bashiru alisema; “jambo la nne ninalotaka kuzungumza ni uwajibikaji, mna nafasi gani ya kusimamia Serikali ili iwe upande wenu, kwa sababu ukweli ni kwamba mamlaka ya Serikali yako mikononi mwa umma na umma ni walio wengi ambao ni ninyi.

“Na vyeo vyote vilivyopo Serikali ni mali yenu, isipokuwa kuna mchakato wa usimamizi wa vyeo vyenu kupitia Serikali na moja ya michakato ni uchaguzi, hebu tujiulize tabia yenu na mwenendo wenu wakati wa uchaguzi ikoje?

“Tuambizane ukweli, mkishapewa kofia na T-shirt (fulana), alafu nyimbo zikaanza kupigwa za ‘mbele kwa mbele’, huwa mnapata nafasi za kuhoji sifa za mnayetaka kumchagua?

“Je, sifa ya chama mnachotaka kukichagua kinachopiga ‘mbele kwa mbele’ unaijua?

“Kwa hiyo eneo jingine muhimu kwa nafasi yenu ni kuwa sehemu ya mchakato ya kuwajibisha wote wenye vyeo vyenu. Kwahiyo msichague kiongozi kwa T-shirt, kwa kofia, kwa ubwabwa, kwa pesa.

“Kwa kufanya hivyo mnatengeneza watu watakaokuja kuwaonea, kwa sababu dhuluma zote na uonevu hazifanywi na wakoloni, zinafanywa na wale mliowachagua nyie wenyewe. Au wale walioteuliwa na wale mliowachagua.

 

“Sasa watu ambao ni wajanja, mimi naweza kusema wapigakura wa Tanzania ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani (siku ya uchaguzi) kwa sababu wanaona ni kama kituko, ni mchezo wa kuigiza.

“Na ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kupiga kura imekuwa shida, kote tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40, hakuna mahala ambako wapigakura wamejitokeza kwa zaidi ya asilimia 50.

“Na mwaka 2010 ilitia fora, watu wengi walijiandikisha zaidi ya asilimia 100, kumbe walikuwa wanataka kile kipatarata (kitambulisho cha mpigakura) kwa sababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, unajitambulisha, walipokipata wakaingia mitini.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tulipata Serikali ambayo haikuwa na uhalali wa kiasiasa kwa sababu wapiga kura wengi zaidi ya asilimia 50 walibaki nyumbani na tatizo hili halijaisha, lakini mwanasiasa akishashinda anasema ushindi ni ushindi tu hata kama ni kwa kura moja.

“Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali, tulifika mahala ambapo ikifika wakati wa uchaguzi wagombea wanauza nyumba, wanakopa, wanaitisha mikutano ya kuchangisha, usipomchangia mkali utafikiri anakwenda hospitali kutibiwa.

“Akishazikusanya zile fedha anaenda kuwanunua mawakala na mawakala wanawanunua wapigakura, msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi, ninachowaomba nafasi yenu ni kubomoa na kuharibu soko la kura.”

Dk. Bashiru alisema kwa sababu kama CCM itakuwa imejipanga, mipango mizuri ya kuhudumia umma ipo, wananchi wanaona shule, hospitali hakuna haja ya kwenda kuhonga.

“Ukiona mtu anakuhonga hana sifa, na ndani ya CCM tumeshasema itakuwa sababu ya kutoteua mtu huyo hata kama atakuwa ameshinda kura za maoni.

“Kwa sababu bila kuwa na mfumo wa kuwapata viongozi, na nasikia sasa hivi rushwa imeenda mpaka kwa wenyeviti wa vijiji, kitu ambacho ni hatari, kwa sababu mwenyekiti wa kijiji anasimamia mazingira na wananchi wake, anasimamia migogoro na wananchi wake, anasimamia haki na wananchi wake, akianza kununua uongozi atauza ardhi.

“Kwahiyo mambo haya manne kwangu mimi naona ni muhimu sana, ili uweze kupata nafasi katika uchumi wa taifa hili, uwezo wenu wa kutambua mambo, kutambua kwamba benki ya ardhi ni wizi, kwamba bodi za mazao ni wizi na mimi nashangaa mpaka leo Bodi ya Kahawa ipo,” alisema.

 

AMSHUKIA WAZIRI WA KILIMO

Dk. Bashiru alisema ameshamwagiza Waziri wa Kilimo, kuvunja Bodi ya Kawaha, lakini anashangaa hatekelezi hivyo kujiuliza ni masilahi gani anayo kwenye suala hilo.

“Nimemwambia waziri vunja hataki, sijui ana masilahi gani huyo, na sijasema mimi, wanaushirika wenyewe, mimi nilikuwa msikilizaji, mwenyekiti wa kikao, wanasema huyu mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa ndiye anayenunua kahawa, anaongoza kununua kahawa kwenye mnada wa soko alafu ni mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa, utapata bei?

“Yaani mwenyekiti wa bodi ndiye mfanyabiashara mkuu, mnunuzi mkuu kwenye soko la kahawa, narudia tena anayehusika na Bodi ya Kahawa akawasikilize wana ushirika wanaridhika na muundo wake na mgongano wa masilahi katika bodi hii?

“Leo mimi Bashiru nikisema, hata ikifuatwa hana maana, semeni nyie kwa sababu na mimi nina ukomo wangu na ukomo ni masilahi yangu kwa sababu mimi ni binadamu pia,” alisema.

 

ARDHI

Akizungumzia suala la ardhi, aliwataka wakulima wadogo kutambua ardhi ni uhai na ni sawa na damu ndani ya mwili wa binadamu hivyo inapaswa kutunzwa, ni uhai wa kizazi hadi kizazi.

Alisema asilimia 90 ya watu wanaofika katika ofisi yake ni masikini ambao wanadai ardhi yao wakati matajiri hawaendi kwake bali wanafika kwa kamishna wa ardhi.

“Kataeni kuuza ardhi yenu kama mnavyojitolea damu kunusuru uhai wa mtu,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema utakuta mwekezaji anapewa eneo kubwa la ardhi na mkulima kubakia kibarua kwa mwekezaji, hivyo kuna hatari kubwa wananchi kugeuka vibarua katika ardhi yao wenyewe.

“Tukianza kuruhusu wawekezaji kuchukua ardhi yote na sisi kubakia hatuna ardhi, tutabaki kuwa masikini na watumwa katika nchi yetu,” alisema.

Dk. Bashiru alisema Serikali inapaswa kurekebisha sheria zote ambazo hazitendi haki.

Alisema msimamo wa Rais Dk. John Magufuli ni ardhi ya nchi hii haitakuwa ya kibiashara na sheria zote kandamizi zitafutwa ama kufanyiwa marekebisho.

 

UCHAGUZI WA 2010

Katika uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa 20,137,303 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapigakura wote waliojiandikisha.

Katika uchaguzi huo, kura zilizoharibika zilikuwa 227,889 ambazo ni sawa na asilimia 2.64 ya kura zilizopigwa.

Katika kura halali 8,398,394 sawa na asilimia 97.36 ya kura zote, aliyekuwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alipata kura 5,276,827 ambazo ni sawa na asilimia 61.17 ya kura zote halali.

Wagombea waliofuatia ni Dk. Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34 ya kura zote halali, huku Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF akipata kura 695,667 sawa na asilimia 8.06.

Peter Mziray wa APPT – Maendeleo alipata kura 96,933 sawa na asilimia 1.12, Hashim Rungwe wa NCCR- MAGEUZI alipata kura 26,388 sawa na asilimia 0.31, Muttamwega Mgaywa wa TLP kura 17,482 sawa na asilimia 0.20 na Dovutwa Nassoro wa UPDP kura 13,176 sawa na asilimia 0.15.

 

CHAGUZI NDOGO

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Ukonga uliofanyika Septemba 16, mwaka huu, waliotarajiwa kupiga kura walikuwa 300,609 lakini waliojitokeza ni watu 88,270 sawa na asilimia 29.4.

Katika uchaguzi huo, Mwita Waitara (CCM), alitangazwa mshindi kwa kupata kura 77,795 sawa na asilimia 89.1, akifuatiwa na Asia Msangi wa Chadema aliyepata kura 8,676 sawa na asilimia 9.95.

Katika Jimbo la Monduli, msimamizi wa uchaguzi, Stephen Ulaya alisema Julius Kalanga wa CCM alipata kura 65,714 sawa na asilimia 95 ya kura zote huku Yonas Laizer wa Chadema akipata kura 3,187.

Alisema walioandikishwa kupiga kura walikuwa 80,282 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 69,521.

Katika uchaguzi wa Jimbo la Buyungu uliofanyika Agosti 12, aliyekuwa mgombea wa CCM, Christopher Chiza alitangazwa mshindi kwa kupata kura 24,578 akifuatiwa na Eliya Michael wa Chadema aliyepata kura 16,910, waliotarajiwa kupiga kura walikuwa 61,980 na  waliojitokeza ni 42,356.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here