32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Fedha inavyoweza kukupandisha au kukushusha

ILI kufanikiwa ni pamoja na kuwa na kanuni nzuri za kupata na kutunza fedha. Lazima ujipange na upitie hatua muhimu zitakazokuwezesha kusogea kwenye utajiri.

Kwa nini tunajifunza mbinu za kuhifadhi fedha? Kwa sababu ni kati ya njia muhimu zinazotumiwa na matajiri wengi kuendelea kuwa matajiri zaidi na kutunza walivyonavyo ili wasiporomoke na kurejea kwenye umasikini.

Mfano kuna wengine wana tabia ya kudharau chenji ndogondogo. Hilo ni kosa kubwa. Ukibaki na chenji katika matumizi yako ya kawaida ya kila siku, acha kuzitumia pasipo sababu ya msingi, hifadhi.

Lakini pia acha kabisa kununua vitu ambavyo havikuwa kwenye mipango. Kuna mtu anaweza kuwa mtaani, akapita muuza mashati, ghafla akamwita na kununua. Siyo utaratibu mzuri kwa mtu mwenye kiu ya kufanikiwa.

Acha kwenda mradi siku zinakwenda, usiishi kama mtu usiye na mipango. Ni muhimu kuwa na bajeti yako ya mwezi, wiki na baadaye kila siku. Bajeti itakusaidia kukuongoza namna ya kutumia fedha zako kwa usahihi. Bila bajeti hutaweza kutunza fedha.

Mwingine anapoteza muda mwingi kuwa barabarani, haina maana. Kuwa na mazoea ya kuwa nyumbani muda mwingi. Kama huna kitu cha lazima cha kuwa nje, ni vizuri kutulia nyumbani.

Kuwa nyumbani kutakusaidia kupanga mipango yako sawasawa. Kuwa nje ya nyumbani pia kutakusababishia uingie kwenye matumizi ambayo hukuwa na mipango yako.

Kama huna akaunti fungua. Ni muhimu sana kuwa na akaunti. Pindi unapopata mshahara wako au faida kwenye biashara zako, chukua kiasi cha fedha na uweke benki. Hii itakupa ahueni na kuishi maisha yasiyo ya presha.

Fedha unazohifadhi zinaweza kukusaidia utakapokuwa na shida muhimu, vinginevyo unaweza kuziacha muda mrefu bila kuzichukua na ukapata faida.

MANUNUZI YAKO YAKOJE?

Unapokwenda kufanya manunuzi yako ni vizuri kuwa na orodha itakayokuongoza. Hii itakusaidia kununua vitu muhimu tu na kama fedha ikibaki unaweza kununua vitu vingine vya burudani kama utapenda kufanya hivyo.

Ukiwa huna orodha, ni rahisi kununua vitu bila mpangilio, mwisho wa siku unagundua kuwa umenunua vitu vingi ambavyo havikuwa vya lazima sana na kuacha vile muhimu.

Kumbuka kutumia fedha kwa ajili ya uvutaji sigara au kunywa pombe, hakuna maana na kunapoteza fedha bila sababu. Mbali na hayo, madhara yanayopatikana kwa utumiaji wa  vitu hivyo ni makubwa na yanahatarisha afya. Kaa mbali na vitu vinavyoharibu afya na endelea kutunza fedha zako.

KUWA MAKINI NA KADI ZA MIAMALA

Kuwa na kadi ya benki au ya kununulia vitu kusikufanye uwe limbukeni wa matumizi yako. Kumbuka hizo ni fedha zako na umehifadhi kwa ajili yako mwenyewe.

Acha tamaa au kutaka kujionyesha kwa watu kuwa unaweza kufanya manunuzi yoyote, muda wowote kwa sababu tu kwenye pochi yako una kadi inayokuwezesha kufanya hivyo.

Ni vizuri kutunza fedha kadiri unavyoweza kufanya hivyo. Utunzaji wa fedha unaweza kukusaidia kukusogeza kwenye mafanikio. Hata kama una fedha ndogo, lakini siku moja utakuja kuwa na fedha nyingi zaidi.

Kwa leo tuishie hapa. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles