27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Fedha dawa za JPM ‘zapigwa dili’

VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM



WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema amebaini kuna ‘mchezo mchafu’ unaofanywa katika halmashauri nchini juu ya fedha za dawa zilizotolewa na Serikali.

Alisema wakati Rais John Magufuli akiwa amejitahidi kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 30 hadi Sh bilioni 270, ambazo zimepelekwa moja kwa moja katika hospitali na vituo vya afya   chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), tangu zilipopata fedha hizo hadi sasa, hakuna halmashauri hata moja iliyorejesha katika Bohari ya Dawa (MSD).

Akifungua bodi mpya ya wadhamini ya MSD jana, Waziri Ummy amemwagiza Mfamasia Mkuu wa Serikali kufuatilia kwa ukaribu suala hilo.

“Nimemwagiza aangalie katika mwaka wa fedha 2017/18 katika kila halmashauri alipeleka dawa na vifaa tiba vingapi, aangalie thamani yake, nataka kuwabana.

“Kimsingi, MSD imetoa dawa za Sh bilioni 200 lakini fedha hazijarudi, MSD ilieleza kwa mfano Ilala mwaka huu tumekuletea dawa za Sh milioni 100 na umeuza rudisha basi asilimia 50.

“Hoja yao ni kwamba wanatoa huduma kwa wagonjwa wa msamaha lakini wagonjwa hao ni asilimia 40, Kwa nini hurudishi ile asilimia 60?

“Unakaa unasubiri mwakani tena wizara ilete fedha nyingine za dawa, yaani Serikalini wanataka kuchukua kwa mkopo lakini akishauza wanasubiri muda ambao MSD dawa zimeisha ndiyo wanapeleka oda kusudi waende kwa watu binafsi kununua.

“Yaani Serikali tunawapa fedha wanazigeuza mtaji kwenda kununua dawa kwa watu binafsi… kwa nini sisi Serikali tugeuzwe mtaji?…kwa nini fedha hazirudi?  Hatuwezi (Wizara) kila siku kwenda kumlilia Rais Magufuli kutupatia fedha za dawa, lazima fedha zilizotolewa zirudi MSD.

Alisema ana matarajio makubwa na bodi hiyo ya wadhamini iliyoundwa, kwamba itahakikisha usimamizi wa fedha hizo za bajeti ya dawa na vifaa tiba unaimarishwa.

“Licha ya mafanikio yaliyopo lakini bado kuna mambo ambayo ni changamoto kwa bodi hii mpya ikiwamo uwezo wa MSD kujiendesha kwa fedha unasimamiwa vema na kuendelezwa ipasavyo.

“Uwepo wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vyenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa vinapatikana kwa gharama nafuu na wakati wote,” alisema.

Alisema bodi hiyo inapaswa kuhakikisha MSD inaendesha shughuli zake kwa gharama nafuu na kupunguza gharama zisizo na tija.

“Kuhakikisha MSD inaziba mianya yote ya rushwa, wizi na ubadhirifu wa aina yoyote ile, kuboresha matumizi ya Teknohama,” alisema.

Alisema nyingine ni kupunguza au kumaliza tatizo la OS (kushindwa kufanya makisio sahihi ya dawa) kwenye vituo vya afya, hospitali za wilaya na zile za rufaa za mikoa.

Alisema malalamiko mengi ni kwamba MSD haipeleki dawa, haipeleki dawa zote zilizoagizwa na mteja na hawatoi mapema taarifa kwa wateja kuwajulisha kutokuwapo  baadhi ya dawa zilizoagizwa.

“Tumebaini kuna changamoto ya quantification yaani dawa zinaletwa nyingi mno kiasi kwamba hivi karibuni imebidi tuzipeleke Zimbabwe ili kuwahi kabla ya muda wa matumizi kuisha,” alisema.

Awali, Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu alimshukuru Waziri Ummy kukamilisha kuundwa   bodi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles