27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Familia ya Diamond ni burudani tupu

CHRISTOPHER MSEKENA

INAWEZA ikakushangaza lakini ukweli unabaki kuwa familia ya Diamond Platnumz, inaongoza kwa kuwa na matukio yenye visa na mikasa inayofurahisha na kufanya iwe familia maarufu zaidi katika anga la burudani barani Afrika.

Ingekuwa kule Marekani mitaa ya Hidden Hills, California, familia ya Diamond tungeifananisha na ile ya mwanamitindo Kim Kardashian ambayo nayo imejaa visa na mikasa inayowaburudisha mamilioni ya mashabiki wanaofuatilia kipindi chao cha runinga, Keeping Up With The Kardashians.

Katika makala haya, Swaggaz tunaangazia maisha ya familia hii ambayo kuanzia wazazi mpaka watoto, wamekuwa kwenye nafasi kubwa ya kuzungumziwa, kutokana na aina ya maisha waliyoamua kuishi kwenye mitandao ya kijamii (Instagram), sehemu wanayoitumia kama njia kuu ya kuwasiliana na mashabiki zao.

MAPENZI

Ndani ya familia hii maarufu, mapenzi yana nafasi kubwa zaidi. Habari nyingi zinazozungumzwa juu yao, zinahusu uhusiano wa mapenzi wa Diamond Platnumz mwenyewe, mama yake Sanura Kassim ‘Mama Dangote’, baba yake Abdul Juma na dada zake Esma Platnumz na Queen Darleen.

Unaweza kuona toka Diamond Platnumz, alipojipatia umaarufu kwenye muziki wa Bongo Fleva, licha ya kufanya ngoma nyingi kali, amekuwa akitumia zaidi mashahiri yenye ujumbe wa mapenzi, unaohusiana moja kwa moja na maisha yake halisi ya malavidavi.

Wanawake ambao amekuwa nao kwenye mapenzi, wamekuwa mtaji kwenye biashara yake ya muziki. Toka ngoma yake ya kwanza iliyomtambulisha ‘Kamwambie’, alimzungumzia demu wake aliyewahi kumtosa kisa hana mkwanja.

Nyimbo zake nyingi zilizofuata baada ya Kamwambie, zilikuwa zina ukweli kwa asilimia fulani kuhusiana na maisha yake ya mapenzi aliyowahi kuishi na warembo mastaa kama Wema Sepetu, Penny, Zari The Boss Lady, Hamisa Mobetto, Tanasha Donna na wengineo.

Mbali na Diamond kutumia mapenzi kama sehemu muhimu ya muziki wake, memba wengine wa familia hii, nao hawapo nyuma. Inafahamika kuwa baba na mama Diamond walishaachana kitambo na ila hivi karibuni wameweka pembeni tofauti zao na kuendelea na maisha huku kila mmoja akiwa na mpenzi wake.

MAMA DANGOTE

Miongoni mwa kapo  zinazoongelewa zaidi kwa sasa ni hii ya mama mzazi wa Diamond na mumewe  Rally  Jones maarufu kama Anko Shamte. Wawili hao wamekuwa wakionyeshana mahaba mazito hadharani, wanagandana kama kumbikumbi katika shughuli mbalimbali.

Jambo linalozua gumzo zaidi ni pale ambapo wawili hao wamekuwa wakipuuza kashfa na maneno ya kejeli kutoka kwa watu wanaosema mama Diamond yupo kwenye dimbwi la mapenzi na kijana mdogo maarufu kama Kibenten.

“Mara nyingi mume wangu huwa ananiita Msweet yaani mtamu kama unavyosikia hapa,” alisikika mama Diamond katika mahojiano aliyofanya na SnS mwezi huu.

Uhusiano huo pia umekuwa kivutio kwa wengi kwani watoto wa mama Dangote  yaani Diamond, Esma na Queen Darleen pamoja na mumewe wa zamani mzee Abdul, wamekubaliana na maisha aliyoamua kuishi mama yao kwa kujiachia mtandaoni.

Hali kadharika mama amekuwa akimuunga mkono mwanawe Diamond  katika kila anachokifanya hata kama atadhalilika. Mama Dangote hajali maneno ya wanaomwona kigeugeu hasa pale anapoonyesha kumkubali zaidi Tanasha kuliko alivyowahi kuwakubali kina Zari na Hamisa Mobetto.

ESMA PLATNUMZ

Kama nilivyosema mwanzoni  mwa makala haya kuwa huwezi kuacha kuizungumzia familia hii kwa namna yoyote ile kutokana na matendo yao. Hivi  karibuni dada wa Diamond, Esma Platnumz aliikwaa skendo nzito ya kumwibia mume msanii toka Zanzibar, Baby J.

Baby J, anasema licha ya kuwa na urafiki na Esma, dada huyo wa Diamond hakulembesha, kwani alimkwapua mume wake na bila kificho amekuwa akijiachia naye mtandaoni na kwenye matukio mbalimbali kama vile  siku ile ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa mama yake na wifi yake, Mlimani City, Julai 7 mwaka huu.

Baby J, hakuishia hapo kwani alihusisha mpaka imani za kishirikina kuwa Esma, ametumia nguvu za giza kumnasa baba wa mtoto wake anayeitwa Aboud Datrinest, kwani mpaka sasa haelewi mbinu alizotumia Esma kumwibia.

Licha ya mashabiki kumjia juu Esma wakitaka arudishe mume wa mtu, mrembo huyo amekuwa kimya na kuendelea kuchapisha picha mtandaoni zikimwonyesha akiwa kwenye mapozi ya kimahaba na jamaa huyo anayedaiwa kuzaa mwishoni mwa mwaka jana mtoto wa kiume na Baby J anayeitwa Danin.

Esma pia amepachikwa jina la Yuda Iskariote, kutokana na usaliti ambao amekuwa akiwafanyia mawifi zake  wa zamani  pindi Diamond anapokuwa kifaa kipya.

BABA DIAMOND BURUDANI KABISA

Baba mzazi wa Diamond, Abdul Juma amekuwa burudani zaidi kutokana na matendo yake anayoyafanya hasa katika mitandao ya kijamii. Kwanza sasa hivi naye ni mwimbaji kama mtoto wake, juzi kati hapa alisikika kwenye moja ya wimbo uliompa umaarufu, ‘Dudu la Yuyu’, kisha akaachia ngoma yake nyingine Unanijua, alioshirikiana na meneja wake Chada Boy.

Baba huyu ni burudani kila siku, ukitazama mambo anayozungumza, jinsi anavyovaa, vile anavyonyoa ni kama vijana wa Bongo Fleva, hiyo inafanya awe gumzo katika jamii kutokana na umri wake kumtupa mkono lakini bado anajiweka kama kijana.

Hata katika mapenzi, mzee huyu sasa ana mpenzi wake anayemwita Neema Ofisa, ambaye amekuwa akiongozana naye katika matukio mbalimbali jambo linaloendelea kuwafurahisha wengi kutokana na maisha anayoyaishi baba Diamond.

Kwa muktadha huo, unaweza kuona ni jinsi gani familia hii imekuwa burudani kwa mashabiki kutokana na matendo yao ambayo haiwezi kupita siku mmoja wao hajawa gumzo kwenye jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles