Na JOSEPH SHALUWA
KATIKA uhusiano wengi hutarajia kuwa na maelewano ili kuwa na matokeo mazuri siku zote. Kwa kawaida uhusiano wenye furaha hutawaliwa na upendo kwa wahusika kwa sababu kila mmoja ana uhakika na penzi la mwenzi wake.
Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, wapo baadhi ya walio kwenye uhusiano, kwa kujua au kutokujua, wanajikuta wakiwaumiza wenzi wao hisia zao na kusabisha misuguano.
Wakati fulani unaweza kumjeruhi moyo mwenzako, lakini yeye asikueleze moja kwa moja, ila kinachotokea moyoni mwake ni kwamba huanza tabia zisizofaa au kufikiria kuchomoka mikononi mwako bila ya wewe kujua.
Waswahili wanasema, moyo wa mtu kichaka! Kamwe huwezi kujua kilichopo ndani ya moyo wa mwenzako kama hajakuambia.
Jambo hilo ni hatari zaidi kwenye uhusiano, maana mwenzako anafanya maamuzi yake, na wewe unakuwa hujui kinachotokea. Kwenye sheria wanasema, kutokujua sheria hakukupi haki ya kutenda kosa husika.
Ukitenda kosa bila kujua, sheria inachukua mkondo wake kama kawaida. Je, unafahamu ni mambo gani yanaweza kujeruhi moyo wa mpenzi wako? Karibu darasani tujifunze.
KUPUUZA MAMBO
Hii ni kwa wote. Wapo baadhi ya wanaume hupuuza mambo ya wenzi wao wakidhani ni madogo, hayana maana. Huenda labda yupo kazini mchana, akatumiwa ujumbe na mpenzi wake wa kumtakia mlo mwema, lakini anapuuza.
Mwenzako amekufikiria na kukutumia ujumbe: “Nakutakia mlo mwema, wenye furaha baby,” halafu wewe unaupuuza. Ni kiasi cha kujibu maneno mafupi tu: “Asante darling kwa kujali.”
Ni mstari mfupi lakini wenye maana sana kwa mwanamke. Huo nimetoa kama mfano tu, lakini yapo mengi. Mwanaume anatakiwa kumjali mwenzi wake hata anapokuwa mgonjwa. Wapo baadhi ambao huendekeza mfumo dume, mwenzake anaumwa, lakini anaendelea kumwachia majukumu yote ya nyumbani.
Kwa hakika siyo utaratibu mzuri. Ikiwa mwenzako anaumwa, unapaswa kujitoa, kuwa karibu yake kwa kila namna. Kujua afya yake ni pamoja na kumpeleka hospitalini, kufuatilia anavyotumia dawa nk.
Unaweza kuona ni mambo madogo, lakini ikiwa atayaweka moyoni, kuna siku anaweza kuchukua maamuzi magumu ambayo hutayategemea. Jenga tabia ya kumsikiliza mwenzako kwa makini, toa ushauri inapobidi na pia tafuta utatuzi wa changamoto anazoeleza.
Kama nilivyosema hapo juu, haya siyo kwa wanaume tu, ni wote wanapaswa kujali na kutokupuuza mambo ya wenzao. Wakati mwingine huenda ikawa hata ushauri tu, lakini namna utakavyochukulia ndivyo utakavyokuwa umejiweka kwa mwenzi wako.
Maumivu yake ni makubwa maana hujui mwenzako anafikiria kufanya nini kutokana na kuumizwa moyo kwa jambo husika.
KUJIWEKA KWENYE MASHAKA
Baadhi ya watu hujisahau na kufanya mambo yasiyo na afya katika uhusiano. Bila kujua anajikuta akifanya mambo ambayo tafsiri yake kwa mpenzi wake siyo nzuri. Kwa mfano, utakuta mtu anawasiliana na mfanyakazi mwenzake wa jinsia tofauti lakini kwa staili isiyo ya kawaida.
Mtu ameoa au ameolewa lakini anawasiliana na mwanaume au mwanamke mwingine, meseji ambazo zina tafsiri mbaya. Huenda ikawa kweli hana uhusiano naye kabisa kimapenzi, lakini namna yao ya kuwasiliana inatia mashaka.
Wanaitana majina ya kimapenzi kama baby, honey, sweetie, mpenzi na mengine kama hayo, ukimwuliza anakujibu tu kwa kifupi: “Ni rafiki yangu tu wa ofisini, hakuna kinachoendelea kati yetu.”
Hivi ni urafiki gani wa kuitana majina ya kimapenzi? Mwingine usiku anampigia simu, akipokea wanapiga stori zisizo na msingi na mwisho eti walikuwa wanasalimiana tu! Nani ambaye atakuelewa?
Kufanya hivyo ni kumjeruhi mwenzako moyo wake, jambo ambalo mwisho wake kwa kawaida huwa siyo mzuri. Lakini kama ni kweli huyo mtu huna uhusiano naye, kwanini ujiweke kwenye hatari hiyo?
Ukishakuwa unamilikiwa, lazima ujiheshimu. Uelewe mipaka yako na ujue kuwa una mpenzi ambaye anakupenda kwa dhati ya moyo wake. Kumuumiza moyo wake kwa namna yoyote ile, huenda kukaleta matatizo makubwa kwenye uhusiano wenu.
Mbaya zaidi ni kwamba, hujui ni kwa kiwango gani utaathiriwa na maamuzi yake, kwa sababu mwisho wa siku, unakuwa moyoni mwake mwenyewe.
Wiki ijayo tutamalizia mada hii, USIKOSE!
Je, ungependa kujifunza zaidi masomo haya kupitia kundi letu la WhatsApp? Karibu inbox ya WhatsApp kwa namba 0718 400146 na ueleze nia yako ya kujiunga na kundi letu, tutakuunga.