29.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

CHUKI ZAO ZISIKURUDISHE MYUMA, SONGA MBELE – 2

Na ATHUMANI MOHAMED


KARIBUNI tena kwenye safu yetu ambayo hutoka kila Jumamosi. Ndugu msomaji wangu, nina imani kuwa wewe ni mzima wa afya na unaendelea vyema kusukuma gurudumu la maisha.

Leo tunamalizia sehemu ya mwisho ya somo tuliloanza wiki iliyopita ambapo tunaangalia namna ya kukabiliana na watu ambao wanakuchukia kwa sababu mbalimbali.

Kama tulivyoanza kuona wiki iliyopita, chuki za watu wengi husababishwa na wivu. Kuwa na uwezo zaidi kikazi, ubunifu, kifedha nk. Sasa leo tumalizie sehemu ya mwisho ya mada hii.

UKWELI HUWEKA HURU

Kufahamu ukweli ni jambo moja la msingi sana katika maisha, lakini kuchukua hatua ni jambo lenye maana zaidi. Kujua sababu ya kuchukiwa ni kitu kizuri sana. Angalau sasa una pa kuanzia baada ya kufahamu ukweli.

Ndugu zangu, ukishagundua kuwa unachukiwa kwa sababu ya tabia zako mbaya, basi ni wajibu wako kubadilisha tabia zako hizo mbaya. Kumbuka unaishi na jamii na ni lazima ukutane nayo katika mambo haya na yale.

Kama wewe ndiye kero kutokana labda na roho mbaya, kuwasengenya wenzako, kuongopa na tabia nyingine za namna hiyo ni wajibu wako sasa kubadilika ili uishi vizuri kwenye jamii inayokuzunguka.

Lakini ikiwa umegundua kuwa unachukiwa kwa sababu kinyume na nilizoeleza hapo juu, pia ni sawa, maana utakuwa umeshaujua ukweli. Mtu kukuchukia kwa sababu ya mafanikio, umaridadi wako, uwezo wako wa kuchangia mada na kadhalika, isikupe shida kabisa.

Kwanini? Nitakupa sababu hapa chini.

BINADAMU NI WABINAFSI

Necha ya binadamu wote duniani ni ubinafsi. Hii ni hulka ya kila mtu. Lakini hata hivyo mtu akiamua huweza kubadilika kitabia au kuficha ubinafsi wake.

Hivyo basi, ieleweke kuwa binadamu yeyote akimuona mwenzake amefanikiwa kwenye eneo fulani, hata kama hatamuonea wivu, lakini moyoni mwake angetamani kuwa na mafanikio kama fulani.

Hakuna mtu ambaye hatamani kuwa kama mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi. Hakuna mtu asiyependa kuwa na utajiri kama wa Said Salim Bakhresa, Mo Dewji au Rostam Aziz; wote hawa mara kadhaa wamekuwa wakitajwa kwenye Jarida la Fobes kama miongoni mwa mabilionea wa Tanzania.

Wapo wasichana wangapi wangependa kuwa kama Wema Sepetu, Irene Uwoya au Jokate Mwegelo? (sasa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe).  Hawa wote walipata kupitia shindano la Miss Tanzania na kuwa na mafanikio makubwa kutokana na umaarufu walioupata kupitia mitindo.

Kuna upande wa wanasiasa pia. Kuna wengi wangependa kuwa kama mbunge au waziri fulani kutokana na namna anavyofanya kazi yake sawasawa. Wakati mwingine mtu anaona kwanini asingekuwa yeye?

Tamaa za namna hii hazina tatizo, lakini ni vibaya kuwachukia kwa sababu eti wamefanikiwa. Mafanikio hayaji yenyewe, hutafutwa tena usiku na mchana.

Hivyo basi, usinyong’onyee moyo wako kwa sababu kuna watu wanakuchukia kwa sababu yoyote ile. Fahamu kuwa binadamu wameumbwa na tamaa ya kuwa na mafanikio.

SONGA MBELE

Dawa kubwa na mujarabu kabisa kwa watu wanaochukia mafanikio ya wenzao ni kuongeza juhudi ili kuendelea kufanikiwa zaidi. Ikiwa labda kazini kwako watu wanakuchukia kwa sababu ni mfanyakazi bora, usirudi nyuma, fanya kazi kwa nguvu zaidi.

Kama kuna mtu anakuchukia kwa sababu unavaa vizuri, endelea kununua mavazi mazuri zaidi ili uendelee kuwaumiza. Hii ni dawa kubwa zaidi, kuliko kurudi nyuma kwa sababu eti unachukiwa.

Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,587FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles