Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIKA historia ya udhibiti wa huduma za nishati na maji, Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetoa bei kikomo inayofanya mlaji wa mafuta ya dizeli alipe Sh 1,600 kwa bei ya Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi bei ya dizeli imeshuka kutoka Sh 1,747 hadi Sh 1,600 likiwa ni punguzo la Sh 147 kwa lita, huku mafuta ya petroli yakishuka kwa Sh 55 hivyo kufanya mafuta hayo kuanzia leo yauzwe kwa Sh 1,842 kutoka 1,898 zilizokuwa zinauzwa mwezi uliopita.
Ngamlagosi, alisema kuendelea kupungua kwa bei za mafuta kwenye soko la ndani kwa kiasi kikubwa kumetokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia, na pia kushuka kwa gharama za usafarishaji, uletaji wa bidhaa za mafuta hayo kuja nchini.
“Hakukuwa na mafuta ya taa yaliyoingizwa nchini katika Mwezi Januari 2016, hivyo katika mwezi Februari 2016 bei ya bidhaa hii itaendelea kuwa kama ilivyokuwa kwa mwezi Januari 2016 ambayo ni S 1,699 kwa lita kwa soko la Dar es Salaam.
“Kushuka kwa namna hii kulitokea mwezi Machi mwaka 2015 ambapo lita moja ya mafuta ya dizeli ilishuka hadi kufikia Sh 145 na kufanya dizeli iuzwe Sh 1,563,” alisema.
Akizungumzia suala la uwiano wa kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na hapa nchini, Ngamlagosi, alisema kushuka kwa bei hapa nchini hakuji siku hiyo hiyo kwa maana kwamba yakishuka leo, kesho yanashuka hapa nchini, bali hutumia kipindi cha miezi miwili kwa bei ya soko la dunia kutumika hapa nchini.
”Aidha ni muhimu kuzingatia kuwa kushuka kwa bei za mafuta masafi (siyo ghafi) katika soko la dunia huchangia takriban asilimia 46 mpaka 49 ya bei katika soko la ndani (kwa bei za Januari 2016), hivyo kushuka huko hakuwezi kuwa na uwiano asilimia 100 kushuka kwa bei katika soko la ndani,” alisema Ngamlagosi.
Pamoja na hali hiyo aliwaomba Watanzania kupuuza uvumi unaoenezwa kuwa EWURA haipendi kushusha bei za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaadhiri mapato (Tozo) ya EWURA. Ukweli ni kwamba tozo ya EWURA inatokana na kiasi cha lita za mafuta kinachouzwa na si kupanda kwa bei.