Na CLARA MATIMO-MWANZA
WATU wengi wamejijengea tabia ya kwenda kununua dawa pindi wanapojihisi kuugua pasipo kupata vipimo na ushauri wa daktari.
Wataalamu wa tiba wanasema tabia hiyo inawaweka katika hatari ya kupatwa na magonjwa mengi bila wenyewe kujijua.
Hivi karibuni Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (CUHAS), kilizindua utafiti wake mpya.
Katika utafiti huo CUHAS kilieleza kuwa kimegundua uwepo wa maambukizi ya bakteria mpya aina ya ‘enterobacter bugandesis’.
Inaelezwa kwamba aina hiyo ya bakteria imeonekana kuwaathiri watoto waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa (njiti) hasa wale walio umri chini ya mwezi mmoja.
Naibu Makamu Mkuu, Taaluma na Utafiti wa CUHAS, Profesa Stephen Mshana, anasema bakteria hao husababisha maambukizi ya ugonjwa (Neonatal Sepsis)
“Matokeo ya utafiti yanaonesha asilimia tano ya watoto walio na umri wa chini ya mwezi mmoja ambao hupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) tayari wameathiriwa na bakteria huyo,” anasema Profesa Mshana.
Chanzo cha bakteria hao
Profesa Mshana anasema kwa kawaida bakteria huyo husababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
“Wananchi wengi wamekuwa na tabia ya kujinunulia dawa kwenye maduka ya dawa na kuzitumia pasipo kushauriwa na daktari, ni hatari na ni vema waache tabia hiyo, lazima wawasiliane na daktari ili apime ijulikane ni ugonjwa gani na waweze kupatiwa matibabu sahihi,” anasema.
Dalili
Profesa huyo anasema bakteria hao husababisha maambukizi ya ugonjwa ujulikanao kitaalamu kama ‘Neonatal Sepsis’.
Anataja dalili zake kuwa ni kupata homa kali, degedege, kupumua kwa taabu na kushindwa kunyonya.
Anasema bakteria hao ni sugu lakini hutibika ingawa matibabu yake ni ghali.
“Chupa moja ya dawa za kutibu ugonjwa huu huuzwa hadi Sh 300,000 na kawaida mgonjwa huhitaji chupa 10 hadi 15 kwa matibabu ya siku saba hivyo mwisho wa siku ukipiga hesabu unakuta kuwa mgonjwa mmoja hugharimu hadi Sh milioni 4.5 za matibabu pekee,” anasema.
Naye Ofisa Mahusiano wa Bugando (BMC), Lucy Mogele, anasema mwaka jana walipokea watoto 240 walio na umri chini ya miezi miwili ambapo kati yao 12 waligundulika kuwa na bakteria hao.
“Kwa mwaka huu pekee tangu Januari hadi Oktoba tumepokea watoto 180 na tisa kati yao waligundulika kuwa na maambukizi,” anasema.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa CUHAS, Profesa Paschalis Rugarabamu, anasema tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 2003 wameweza kupata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa tafiti bora kama hiyo.
“Chuo kimeweza pia kutoa madaktari bingwa 111 na kati yao wamo wa magonjwa ya akina mama, afya ya watoto, utabibu na upasuaji ingawa idadi hiyo haikidhi mahitaji ya taifa,” anasema Profesa Rugarabamu.