26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu ya ufundi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi-RC Kafulila

Na Samwel Mwanga, Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila amesema kuwa elimu ya ufundi inayotolewa katika Vyuo vya Ufundi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwani inazalisha vijana ambao wanakuwa na maarifa makubwa.

Sehemu ya jengo la Utawala likiendelea na ujenzi katika Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu kinachojengwa eneo la Bunamala mjini Bariadi.(Picha Na Samwel Mwanga).

Pia amesema mafunzo ya elimu ya ufundi yana nafasi kubwa ya kuongeza, kusaidia  na kukuza ajira kwa vijana wanaosoma masomo hayo kwenye hivyoi  kwa kuajiriwa au kujitengenezea ajira wao wenyewe.

Kafulila amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi unaoendelea wa Chuo  cha Elimu na Mafunzo Ufundi Stadi (VETA)mkoa wa Simiyu kinachojengwa eneo la Bunamala mjini Bariadi.

Amesema kuwa tafiti nyingi zinaonyesha mataifa yaliyopiga hatua katika mapinduzi ya kiuchumi zimewekeza katika vyuo vya ufundi vya kati na màtokeo yake ni makubwa sana huku akitolea mfano wa nchi za Korea Kusini, Vietnam na India.

Amesema wanaosoma kwenye vyuo hivyo wanakuwa wakifanya kwa vitendo kutokana na kuwa na maarifa zaidi ukilinganisha na wale wanaosoma vyuo vya kitaaluma tu kwa muda mrefu.

“Watu wanaosoma vyuo hivi vya ufundi wana maarifa zaidi kuliko wale wanaosoma vyuo vya kitaaluma zaidi kwa sababu wanatumia muda mwingi kufanya kwa vitendo,” amesema Kafulila.

Amesema kutokana na hali hiyo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu imekuja na mabadiliko makubwa kwa kuwekeza katika vyuo vya elimu ya ufundi vya kati kwa kujenga vyuo 25 vipya vya VETA na mkoa huo ukinufaika kwa kujengewa chuo hicho.

“Hiki ambacho Rais amekifanya cha kuhakikisha anawekeza katika vyuo vya kati vya elimu ya ufundi na sisi Simiyu tukiwa wananufaika ,ndicho kilifanywa na nchi kama Korea Kusini,India na Vietnam na kwa sasa nchi hizo zimeendelea sana.

“Ni matarajio yangu makubwa vijana watakaomaliza katika chuo hiki watajiajiri na tutakuwa na mafundi wa kutosha maana kwa sasa kuna miradi mingi ya ujenzi inayotolewa na serikali katika sekta ya afya,elimu,maji na miundo mbinu ya barabara na hapa Simiyu wengi hawana sifa hadi wanatoka mikoa jirani ya Mwanza na Shinyanga ila kwa sasa tatizo hili litakwisha kupitia chuo hicho,”amesema.

Aidha, amesema kwa sasa malengo  makubwa  ya serikali ni kuinua ubora wa mafunzo yanayotolewa na vyuo vya ufundi, kuinua umuhimu  mafunzo ya ufundi na jinsi inavyoweza kusaidia kwenye maendeleo ya kukuza uchumi nchi.

Naye, Mhandisi Jalalya Mabojano ambaye ni Mshauri Elekezi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi huo amesema kuwa ujenzi huo unatarajia kuwa na majengo 25 na uwezo wa kuchukua wanafunzi 320 wa bweni ambapo wavulana 160 na wasichana 160.

Mhandisi Mabojani amesema kuwa ujenzi huo unatarajia kukamilika Agosti 30 mwaka huu na mwezi Septemba mwaka huu mafunzo ya muda mfupi yataanza kutolewa chuoni hapo na Mwezi Januari mwakani yataanza mafunzo ya muda mrefu.

“Ujenzi ni lazima ukamilike Agosti 30, mwaka huu na ifikapo mwezi Septemba, mwaka huu mafunzo ya muda mfupi yataanza na mwezi Januari mwakani yataanza mafunzo  ya muda mrefu na hilo linawezekana kwani fedha ipo hakuna shida,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles