Na Salome Bruno, Tudarco
Kwa kumekuwa na mavazi ya kila aina ambayo yanapendwa na wadada wengi hasa wakati huu wa utandawazi. Yapo ya kushona kwa vitenge, vitambaa na uzi wa kufuma pamoja na zile za kununua dukani zikiwa tayari.
Kawaida nguo nyingi hubuniwa na wabunifu mbalimbali, wapo wadogo na wakubwa kutoka nchi tofauti.
Kwa sasa nguo za kushona zilizoshika chati kwa hapa nchini na kupendwa na wasichana wengi hasa wa mjini ni Elastic.
Elastic ni aina ya nguo inashonwa kwa kitambaa au kitenge lakini kwa ndani inaongezewa mpira ‘lastic’ na kuifanya iwe inavutika, hivyo kuvaliwa na mtu wa umbo lolote.
Mwanadada Siya Mwalingo maarufu Cyatrends ambaye ni mbunifu amezungumza na Mtanzania Digital na kuelezea nguo hizo na sababu zinazopendwa kwa sasa.
Siya amesema aina hiyo ya mavazi inapendwa kutokana na utofauti na nguo nyingine za kushona zilizozoeleka.
‘’Nilichagua ‘elastic’ kwa sababu ni za kitofauti na siyo kila fundi anauwezo wa kuzishona kama kushona hizi nguo za kawaida, nashukuru mafanikio ni mazuri na nguo zangu zinapendwa ndani na nje ya nchi,”amesema Siya.
Aidha amesema changamoto ni nyingi, mfano alitarajia makubwa lakini janga la Corona likaathiri biashara kwa sababu kuna baadhi ya malighafi hazipatikani sokoni tena.
Ushauri wake kwa vijana ni kuwa wabunifu na kuacha kutegemea ajira za kuajiriwa katika taasisi bali wajiajiri.