REDIO ya Efm kupitia kipindi chake kipya cha Uhondo imeandaa shindano maalumu la kanga kwa ajili ya wanawake wanaosikiliza redio hiyo.
Shindano hilo litaanza Septemba 14 hadi Oktoba 5, mwaka huu, likiwa na lengo la kuwahamasisha wanawake wafuatilie kipindi hicho kwa kuwa kina faida nyingi kwao.
Msemaji wa redio hiyo, Dennis Sebbo, alisema washiriki wa shindano hilo watatakiwa kubuni maneno ya kanga kupitia kipindi cha Uhondo na maneno yanatakiwa yawe na neno Uhondo, mfano; “Uhondo wa ngoma uingie ucheze”, na mshindi atajinyakulia shilingi milioni moja za Tanzania.
Sebbo aliongeza kwamba pia wamelenga kuinua uchumi wa mwanamke kwa kumpa elimu ya ujasiriamali kupitia mradi wa kanga badala ya kukaa nyumbani bila faida ya msingi.
Kipindi cha Uhondo kinachorushwa kuanzia saa sita mchana hadi saa tisa alasiri, kinaendeshwa na Dina Marios na Swebe Santana, anayejiita Rais wa wanaume.