Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekifungia Chuo Kikuu cha Eckernforde na taasisi zake kutokana na kuwa wadeni sugu wa kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE), kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kuendeleza ufundi stadi (SDL) tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2016.
Meneja wa Mapato wa TRA, jijini humo Masawa Masatu amesema hayo leo baada ya kufungwa kwa chuo hicho ambapo pia mamlaka hiyo imeifungia Hoteli ya Tanga huku Meneja huyo akisisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu hadi wadaiwa wote sugu watakapolipa madeni yao.
“TRA imechukua hatua ya kufungia majengo yote matano yanayomilikiwa na taasisi hiyo ya elimu baada ya kubainika kuwa ni wadeni sugu na wamekuwa wakikaidi ulipaji kodi kwa miaka mingi,” amesema Masatu.
Hata hivyo, Meneja huyo alipotakiwa kutaja kiasi cha fedha inachodaiwa taasisi hiyo amesema taratibu haziruhusu kutokana na sheria ya takwimu kumbana.
Naye Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kiango amesema hali hiyo imesababishwa na chuo kukosa wanafunzi kwa ambapo mwaka huu wa masomo kimepokea wanafunzi wachache huku wafanyakazi wa Tanga Hoteli wakilalamika kutolipwa mishahara tangu Julai, mwaka huu.