26.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

DUWASA watakiwa kuendelea kuwa wabunifu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Hamisa Kalombola ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuendelea kuwa wabunifu ili kuhakikisha majisafi na salama yanapatikana wakati wote.

MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mst. Hamisa Kalombola (wa tatu kulia) pamoja na Makamishna wakimsikiliza Mwandisi wa Uzalishaji Maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Peter Shemwelekwa, akielezea mfumo wa kieletroniki wa uzalishaji maji wakati wa ziara ya Makamishna wa tume katika Mamlaka hiyo jijini Dodoma jana. Wapili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph. (Picha na Mpigapicha Wetu)

Ameyasema hayo Septemba 29, 2022 wakati wa ziara ya kikazi ya makamishna wa tume hiyo katika ofisi za DUWASA ambapo alizungumza na menejimenti ya Mamlaka hiyo.

“Mamlaka yenu iendelee kufanya tathmini ya mipango yake ili uwekezaji unaofanyika uwe na matokeo chanya na lengo la Serikali la kuwaletea watanzania ustawi wa maendeleo liweze kufikiwa,” alisema Jaji Mstaafu Hamisa

Pia, aliwataka watumishi kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu, uzembe, wizi, ubadhilifu, uombaji wa rushwa ili wananchi wapate huduma bora.

“Mtaweza kujiepusha kutenda makosa kwa kuhakikisha wakati wote mnatekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu,” alisema Jaji mstaafu Hamisa

Naye Kamishina wa Tume hiyo, Susan Mlawi alisema wao kama tume wana jukumu la kuweza kufahamu mazingira ambayo watumishi wanafanya kazi ikiwa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma zinazingatiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema kwa sasa miradi ambayo inahitajika kutekelezwa kwa uharaka ni kupeleka maji mjini Dodoma kwa kutumia bwawa la Mtera wakati ikisubiriwa maji ya Bwawa la Farkwa au ziwa Victoria ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu.

Alisema mahitaji ya maji kwa Jiji la Dodoma ni lita milioni 133 kwa siku lakini yanayozalishwa kwa sasa ni lita milioni 67 hivyo kuna upungufu wa lita milioni 66  lakini mradi wa maji kutoka Bwawa la Mtera unatarajia kuingia lita 68 na kufanya jiji liwe na lita 201 milioni ambayo yatatosha kwa matumizi walau kwa miaka 13 ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles