NA EDSON NGOGO,
DUBU ni miongoni mwa wanyama wakubwa wawindaji na wala nyama, kimuonekano unaweza kumchukulia kawaida na ukahisi labda ni mnyama anayekula majani tu, lakini ukweli ni kwamba mnyama huyu ni hatari na ni miongoni mwa wanyama wenye sifa ya kurarua. Dubu dume huwa mkubwa zaidi ya jike, uzito wao huwa kilo 350 mpaka 700 inategemea na afya na umri wake, kutoka mkiani hadi kichwani huwa na mita mbili na nusu mpaka mita tatu na nusu, viungo alivyo navyo kichwani ni vya kawaida yaani macho ambayo huwa madogo, pua huwa kubwa kidogo na masikio si makubwa sana isipokuwa mdomoni kwake huwa na meno 42.
Uwezo wake wa kunusa ni mkubwa mno, anaweza kulitambua windo lake hata akiwa umbali mkubwa kutoka alipo na hiyo ni kwa sababu ya kuwa na pua inayofanya kazi vyema.
Licha ya kwamba ni mnyama anayezaliwa nchi kavu, ni fundi mzuri wa kuogelea na mpenzi wa kushinda majini. Hivyo huwa anawinda nchi kavu pia baharini na chakula kikuu apendacho ni fisi maji, ambao huwakamata kwa urahisi kutokana na uzembe uliopitiliza, hata hivyo mawindo yake hutumia akili nyingi.
Ni heri upambane na simba lakini si dubu, katika hili nyati ni mfano, wanapomuona dubu hukimbia bila hata kugeuka nyuma na hata akikamata mtoto wake humuachia huku wao wakiangalia namna ya kujiokoa, wakati katika hali kama hiyo hiyo kwa simba huamua kumgeukia, kwa mbio ambazo hutimua wamuonapo dubu unaweza kufikiri wamechanganyikiwa.
Ingawa dubu ni mnyama mzito na mwenye mwili wenye muonekano wa kizembe, anaouwezo mkubwa wa kukimbia, si rahisi kuhisi kama unaweza shindana naye kukimbia na ukamshinda, miguu ya mnyama huyu humpa uwezo mzuri wa kujimudu kwakuwa ni mizito na yenye nguvu.
Wanyama hawa miaka yao ya kuishi duniani ni kama walivyo wanyama wengine walao mnyama, huishi kati ya miaka 14 hadi 17 na kwa bahati wengine hufika hadi miaka 20, miili yao imefunikwa na vinyweleo ambavyo huweza kufikia sentimita 15, usawa wa nusu rula ambapo vinyweleo hivyo kwa kiasi fulani humsaidia kujikinga na baridi, hata hivyo mnyama huyu hupatikana sehemu ambazo zina baridi kali. Kuna wakati huogelea katika maji ambayo yana vipande vya barafu, katika hili inathibitisha kwamba baridi kwake ni jambo la kawaida.
Kwa bahati mbaya wanyama hawa hawapo hapa nchini, hupatikana katika mataifa mengine kama Urusi, Kanada, Norway, Marekani na baadhi ya sehemu zingine ambazo huwa na baridi kali inayochangia kutanda kwa barafu, mnyama pekee anayemuwinda dubu ni binadamu. Kama ilivyo kwa wanyama wengine kama tembo, twiga, mamba na wengineo dubu pia huwindwa na majangiri.