NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amemkabidhi timu ya Dodoma FC Mkuu mpya wa Mkoa huo, Dk. Benelith Mahenge.
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, alifanya mabadiliko kwa wakuu wa mkoa ambapo Rugimbana aliondolewa na Dk. Mahenge akibadilishwa kutoka mkoani Ruvuma na kwenda Dodoma.
Dodoma FC inashiriki Ligi Daraja la Kwanza ambapo mpaka mzunguko wa kwanza ulipomalizika juzi timu hiyo inaongoza kundi C kwa kujikusanyia  pointi 18.
Akizungumza juzi mjini hapa wakati wa makabidhiano ya ofisi, Rugimbana alisema anaondoka Dodoma lakini mojawapo ya majukumu anayomwachia Dk. Mahenge ni kuhakikisha Dodoma FC inapanda  ligi kuu.
Rugimbana alisema makao makuu ya nchi yameshahamia Dodoma, hivyo ni lazima kuwe na timu ya ligi kuu.
Alisema timu ya Dodoma FC inashiriki Ligi Daraja la Kwanza, hivyo ni lazima aipe ushirikiano wa hali na mali ili iweze kufanya vizuri katika ligi hiyo.