31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Slaa: Tutawashitaki The Hague wavunjifu haki za binadamu

DK-SLAANa Mwandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vilivyotokea miaka ya nyuma nchini.
Kwa mujibu wa mtandao wa Chadema Diaspora, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika mkutano na wanasheria 12 wakubwa nchini Marekani, uliofanyika Bloomington Jimbo la Indiana kuhusu matukio makubwa ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyogusa jumuiya ya kimataifa.
Dk. Slaa ambaye yuko ziarani nchini humo, alisema watu wote watakaokutwa na hatia watapelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi, lengo ikiwa kuifanya dunia iishi kwa amani.
“Haki nchini Tanzania iko kwa watawala. Watu wa kawaida hawaipati, hali hii lazima ikomeshwe. Familia ya mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi inahitaji haki. Waliomteka aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Stephen Ulimboka lazima wapatikane. Walioua watu kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika Arusha lazima walipe kwa uhalifu wao. Nimeguswa na moyo wenu kwa Tanzania. Hili ndilo lengo letu na kwa dunia nzima iishi kwa amani,” alisema Dk. Slaa.
Naye Dk. Richard Kruss wa Kituo cha Sheria cha Ahlers & Cressman PLLC alisema jinsi nchi inavyoelekea kwenye uchaguzi mkuu kunakuwa na uvunjifu wa haki za binadamu.
Dk. Kruss na taasisi yake, wameahidi kuongoza timu ya wataalamu wa sheria na mashirika ya haki za binadamu kuhakikisha wote waliohusika na uhalifu wanawajibishwa.
“Tutafanya kazi kwa karibu na Taasisi ya Amnesty International, wanaharakati, taasisi za haki za binadamu, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita na wataalamu wa sheria wa Chadema kuorodhesha matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu nchini Tanzania,” alisema Dk. Kruss.
Alisema timu yake pia inakusudia kutoa mafunzo ya sheria kwa wanasheria wa Chadema miezi michache ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles