Na Mwandishi Wetu- Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka mabalozi wapya wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchi za nje kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda ambayo ndiyo kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa.
Kauli hiyo aliitoa Ikulu mjini hapa jana wakati alipofanya mazungumzo na mabalozi wateule waliofika Ikulu kumuaga pamoja na kufanya naye mazungumzo na alisisitiza kuwa sekta ya viwanda imepewa kipaumbele na kutiliwa mkazo mkubwa na Serikali zote mbili.
Miongoni mwa mabalozi aliokutana nao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil, Balozi Mbelwa Kairuki anayekwenda China, Balozi George Madafa, anayekwenda Italia, Balozi Profesa Elizabeth Kiondo, anayekwenda Uturuki.
Wengine ni Balozi Dk. James Msekela anayekwenda Uswisi, Balozi Samwel Shelukindo, anayekwenda Ufaransa na Balozi Luteni Jenerali (mstaafu), Paul Mella, anayekwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Dk. Shein alisema shabaha kuu ya Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha sekta ya viwanda vikiwamo vikubwa, vidogo na vya kati na akawataka kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi hizo wanazokwenda kufanyia kazi.
Akizungumzia kwa upande wa Zanzibar, alisema licha ya Zanzibar kuwa ni kisiwa sambamba na kuwepo ukanda wa bahari kutoka Tanga hadi Mtwara, lakini maeneo hayo hakuna viwanda vya samaki ambayo ni bidhaa inayotokana na bahari.
Alisema eneo la bahari la Zanzibar ni maarufu kwa samaki aina ya jodari anayependwa duniani, lakini wamekuwa hawavuliwi ipasavyo na badala yake hutokea meli kubwa za kigeni za uvuvi ambazo huja kuwavua kwa njia za wizi.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya ajira na kupunguza changamoto iliyopo katika sekta hiyo hapa nchini hasa kwa vijana.
Pia aliwataka mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na Tanzania nzima kiutalii ambapo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo imekuwa ni muhimu kutokana na kuchangia asilimia 80 ya pato la Taifa.
Kwa upande wao, mabalozi hao walimthibitishia Dk. Shein kuwa wamepokea maelekezo yote aliyowapa na kuahidi kuyafanyia kazi hasa kwa maeneo maalumu ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Akitoa maelezo kwa niaba ya wenzake, Dk. Nchimbi, alimhakikishia Dk. Shein kuwa watafanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa kwa masilahi ya nchi yao na wananchi wake.
Pia walimweleza Dk. Shein kuwa watahakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo na Tanzania unaimarishwa zaidi.