Na Mwandishi Wetu, Unguja
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar (ZHELB) kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kusimamisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi hadi Serikali itakapojiridhisha na utaratibu wa utoaji wake.
Dk. Shein ametoa agizo hilo jana ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Dk. John Magufuli kuibua madudu matano yaliyosababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokosa mikopo ya elimu ya juu.
Akizungumza juzi wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Magufuli aliyataja madudu hayo kuwa ni utaratibu mbovu serikalini, kutokuwapo kwa uratibu wa kufungua vyuo, mawasiliano duni kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), wanafunzi wasiokuwa na sifa kupewa mikopo na kile alichokiita utitiri wa vyuo vikuu nchini.
Lakini licha ya changamoto hizo, Rais Magufuli alisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi wa elimu ya juu mwenye sifa atakayekosa mkopo.
Naye Dk. Shein akizungumza mjini hapa jana katika hafla ya utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne mwaka jana na kidato cha sita mwaka huu, alisema katika utaratibu wa sasa wapo waliodanganya kupata mikopo, lakini wamekuwa wagumu kuirejesha.
“Hatutatoa mikopo mwaka huu hadi hapo tutakapokamilisha kazi ambayo tumeanza kuifanya ya kupitia upya utaratibu wa utoaji mikopo hiyo, ili kuhakikisha inatolewa kulingana na mahitaji ya sasa ya nchi na kwa wanaostahili,” alisema Dk. Shein.
Katika halfa hiyo iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Usii Gavu, jumla ya wanafunzi 119 waliomaliza kidato cha nne na 50 waliomaliza kidato cha sita walipewa zawadi kwa kupata daraja la kwanza.
“Wapo waliokejeli matokeo yenu, lakini ukweli ni huo, mpo 50 wa kidato cha sita mliopata daraja la kwanza na wengine 119 mliofaulu daraja la kwanza mtihani wa kidato cha nne,” alisema Dk. Shein.
Alisema ufaulu wa wanafunzi hao ni sifa kwa Zanzibar na anaamini kwa hatua zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha miundombinu ya elimu na rasilimali watu kitaongeza kiwango cha ufaulu.
“Mnapofanya mitihani sote tunakuwa na wasiwasi; nyinyi wenyewe, walimu, wazazi na Serikali kwa kuwa tunaelewa kuwa matokeo yoyote ni yetu na kama ni mazuri ni furaha yetu sote na kama si mazuri ni huzuni yetu sote,” alisema Dk. Shein.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alimhakikishia Dk. Shein kuwa wamejizatiti kuhakikisha sekta ya elimu inazidi kupata mafanikio pamoja na kuwepo changamoto kadhaa.