25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Utata mamilioni ya Lipumba

1

Na EVANS MAGEGE,

NI shida! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Ibrahim Lipumba, kuamua kukiendesha chama hicho kwa fedha zake za mfukoni.

Haijajulikana mara moja Profesa Lipumba anakopata fedha hizo, lakini yeye mwenyewe amekuwa akiwaambia watu wake wa karibu kuwa ni malipo yanayotokana na kazi zake za kushauri masuala ya uchumi katika ngazi ya kimataifa.

Taarifa za uhakika na ambazo gazeti hili limezinasa, zinaeleza kuwa hata ziara aliyoifanya hivi karibuni katika baadhi ya mikoa ikiwamo Lindi na Mtwara, imefanikishwa kwa mamilioni ya fedha zilizotoka katika mfuko wa Prof. Lipumba.

Aliporejeshwa tu katika nafasi yake ya uenyekiti na Jaji Francis Mutungi, ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Profesa Lipumba alikaririwa akisema alikuta akaunti ya chama hicho ikiwa haina senti hata moja.

Hata hivyo, alisema suala la fedha ndani ya chama hicho linasimamiwa na Bodi ya Wadhamini wa chama pamoja na Katibu Mkuu, Maalim Seif, ambaye anatambuliwa kama ‘mhasibu mkuu’.

Mbali na taarifa hizo, madai mengine yaliibuka hivi karibuni yakimtuhumu Profesa Lipumba kufungua akaunti benki kwa lengo la kuingiziwa fedha za ruzuku, jambo lililopingwa vikali na Baraza la Wadhamini, likisema ni kinyume cha sheria na kwamba mkakati huo una taswira ya kuwavuruga.

Taarifa za sasa za kiongozi huyo kutoa fedha zake mfukoni, zimethibitishwa pia na msaidizi wake wa karibu, Abdul Kambaya, ambaye anashikilia wadhifa wa Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa chama hicho.

Kambaya ambaye anatajwa kama msiri mkubwa wa Prof Lipumba, alikiri kiongozi huyo kutumia fedha zake za mfukoni, akisema amelenga kutekeleza dhamira yake ya kutibu majeraha yaliyotokana na msuguano uliopo kati yake na baadhi ya viongozi wa chama chao.

Alitoa ufafanuzi huo baada ya MTANZANIA Jumapili kuhoji chanzo cha fedha zilizowezesha ziara ya kisiasa ya Prof. Lipumba aliyoifanya hivi karibuni.

Akizungumza kwa sauti ya ukali kidogo, Kambaya alisema bajeti ya ziara ya Prof. Lipumba katika mikoa hiyo ilikuwa ni shilingi milioni tatu, kiasi ambacho si rahisi kwa mwenyekiti huyo kushindwa kukimudu.

“Ah! Wanaohoji Profesa Lipumba kutoa fedha CUF ni wajinga tu, kwani mara ngapi Profesa kakisaidia chama? Kwani wakati chama kinafanya kampeni mwaka 1995 wakati huo chama hakikuwa na ruzuku walihoji hilo? Ndiyo, nasema huo ni ujinga tu, hoja zao za kipuuzi puuzi tu, Profesa si mtu wa kushindwa kuwa na Sh milioni 30, 40 hata 50,” alisema Kambaya.

Alikwenda mbali zaidi na kuzungumzia suala la akaunti ya CUF, akipinga taarifa zinazodai kuwa ipo chini ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika hilo alisisitiza kuwa suala la fedha lipo chini ya chama na linasimamiwa na Bodi ya Wadhamini.

“Ndiyo maana nasema ujinga kwa sababu hata hiyo akaunti ya CUF haipo chini ya Katibu Mkuu, akaunti haiwezi kuwa chini ya Katibu Mkuu, kwani Katibu Mkuu ndiyo chama? Akaunti iko chini ya chama, kwani akifa huyo Seif ndiyo chama hiki hakiendi? Kwamba ameshakufa yeye na akaunti anayo yeye kwa hiyo chama hakipo?

“Ninachosema Profesa ana uwezo yeye mwenyewe wa kifedha na kakisaidia sana chama hiki. Na hii bajeti ya juzi ni Sh milioni tatu, hivi milioni tatu Lipumba hana?

“Profesa hakuanza leo kukisaidia chama, haya magari sita yaliyoingia kwenye kampeni alikopesha pesa zake dola elfu 50, mbona hawasemi? Kwa sababu ya mambo ya kiutendaji hatuwezi kusema vitu vingi, kawanunulia Radio Mwambao iko Tanga kwa kuwakopesha dola elfu 50 nyingine, mbona hawahoji? Na sijui kama wamemrudishia hizo fedha na ujue fedha hizo si za madafu, dola elfu 50 ni takribani Sh milioni 100 na ushee, mbona watu hawahoji hilo?” alisema Kambaya.

Wakati Kambaya akisema hayo, hivi karibuni yaliibuka mabishano kuhusu uamuzi wa Profesa Lipumba kutaka kufungua akaunti nyingine ya chama hicho.

Mazingira hayo pia yalimsukuma Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro, kufafanua kwamba wenye mamlaka halali ya kufungua akaunti ya chama hicho ni bodi yake ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif.

“Tunatoa onyo kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwamba tumeshafungua shauri na utaratibu wa kisheria umeshaanza kuchukua mkondo wake, tumesikitika kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kinyume cha sheria namba tano 1992 ya vyama vya siasa na kinyume cha katiba, Msajili kwa mara ya kwanza anaziandikia benki zilizosajiliwa na BoT akizitaka kumfungulia akaunti Lipumba za kuwekea fedha,” alisema Mtatiro.

Alidai kuwa benki itakayomfungulia akaunti Lipumba itakuwa inafanya makosa makubwa.

“Kwa sababu huwezi kufungua akaunti ya taasisi au chama bila bodi yake ya wadhamini kukaa kikao na kuandaa muhtasari kwa ajili ya kupeleka benki ili kufungua akaunti. Lipumba na watu wake wameandaa nyaraka feki pamoja na barua ya Msajili kutaka kufungua akaunti. Tunajua amepeleka katika benki mbalimbali.

“Benki ya National Microfinance (NMB), ilikataa, sasa wanapeleka benki ya Exim na ilishapewa taarifa kuwa uhuni huu haukubaliki na masuala ya fedha yako chini ya katibu mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF,” alikaririwa Mtatiro.

MADIWANI CUF WASHIKANA MASHATI

Kutoka Tanga, Mwandishi Wetu Amina Omari anaripoti kuwa madiwani wa chama hicho katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, wamelazimika kushikana mashati baada ya miongoni mwao kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani na kusaini posho, huku wengine wakiendelea na mgomo wa kutomtambua Meya wa Jiji hilo.

Vurugu hizo zilizotokea katika ofisi za chama hicho Wilaya ya Tanga, zilizotokana na madiwani hao kugawanyika makundi mawili ya walioridhia kuendelea na shughuli za halmashauri hiyo na wale waliogoma.

Hali hiyo ilitokea katika kikao cha Kamati ya Utendaji Wilaya kilichoitishwa kujadili mustakabali wa madiwani walioamua kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Oktoba 12, mwaka huu.

Vurugu hizo zilianza baada ya Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwanzage na ambaye aligombea nafasi ya Meya, kuamuru madiwani waliohudhuria baraza watoke nje ili wajumbe waanze kumjadili mmoja mmoja.

Ndipo kundi la madiwani 12 waliotolewa nje kusubiri kuhojiwa lilipoamua kuingia kwa nguvu kutaka kumtoa Jumbe wakidai kwamba anasababisha makundi ndani ya chama hicho.

Waandishi wa habari walishuhudia vurugu zikiendelea kwenye mlango wa kuingilia katika ofisi hiyo jambo lililosababisha wanachama waliokuwa nje nao kuingilia kati huku wakirushiana ngumi.

Baadaye magari matatu yaliyokuwa na askari wa Jeshi la Polisi yaliwasili eneo hilo na kuwatawanya wanachama waliokuwa wamejaa ofisini hapo.

Katibu wa CUF Wilaya ya Tanga, Thobias Haule ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mnyanjani, alisema ukweli ni kwamba  madiwani 12 waliohudhuria kikao cha Baraza la Madiwani hawakwenda kinyume na chama kwa sababu waliamua kuwawakilisha wananchi waliowachagua badala ya kuendeleza mgomo ambao hauwasaidii.

“Tukubali kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja tulichokaa bila kushiriki vikao vya baraza kuna mambo mengi ya maendeleo ya wananchi ambayo  hayakufanyika, tumeamua kuhudhuria kwa masilahi mapana ya wananchi,” alisema Haule.

Kwa upande wake Mbunge wa Tanga, Mussa Mbarouk (CUF), alisema kuwa anashangazwa na maamuzi yaliyochukuliwa na kamati ya utendaji ya chama hicho kwani walikubaliana madiwani wote walioshiriki kikao cha baraza wahojiwe kwenye mkutano mkuu na si mmoja mmoja.

Hata hivyo aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito kwani viongozi wake wako imara na hawatakubali kuyumbishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles