Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa miezi miwili kwa taasisi zote zinazohusika na ujenzi wa ofisi ya Zimamoto zinazojengwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, ziwe zimekamilisha ujenzi huo.
Agizo hilo alilitoa jana baada ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Zimamoto katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, ujenzi ambao unaonekana kusuasua kwa muda mrefu.
Dk. Shein alizitaka taasisi husika kukamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi hicho hasa ikizingatiwa wahusika walipewa agizo hilo Mei mwaka jana wakati alipotembelea uwanja huo.
Alisema tangu kipindi hicho hadi leo ujenzi huo haujaanza na kusisitiza ni lazima ukakamilike katika kipindi hicho hasa ikizingatiwa serikali imekwisha kutoa Dola za Marekani milioni 3.5 kwa ajili ya ununuzi wa gari za zimamoto na dola milioni 1.5 ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya nununuzi wa gari hizo.
“Tusifanye kazi kwa utamaduni tuliozoea, nimekupeni muda mrefu miezi miwili, malizeni mkimaliza nitakuja, hamkunialika nitakuja mkinialika nitakuja…fedha zipo lakini hamjaziomba,” alisema Dk. Shein.
Waziri wa Ncho Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir alimueleza Dk. Shein haja ya kuwapo ushirikiano kwa taasisi zote zinazosimamia ujenzi huo.