RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, jana aliongoza maelfu ya wananchi visiwani humo kushiriki mazishi ya mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Hamid Ameir.
Hamid Ameir ambaye alifariki jana katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar, alikokuwa amelazwa, amezikwa kijijini kwao Donge Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akisoma wasifu wa marehemu,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alisema marehemu alishiriki kikamilifu Mapinduzi yaliyowakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka kwa wakoloni mwaka 1964.
alisema marehemu alizaliwa Januari mosi, 1928 alijiunga na Chama cha Afro Shirazi mwaka 1957 na kushiriki kuunda Umoja wa Vijana wa chama hicho (ASPYL).
Alisema marehemu alishika nyadhifa mbalimbali katika Serikali na Chama cha Afro Shirazi na baadae Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia aliwahi kuwa kamanda wa Jeshi la Ukombozi na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Viongozi wengine wa kitaifa walioshiriki mazishi ya mwasisi huyo, ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wa dini.
Kutokana na kushiriki kwake mapinduzi na kwa mchango wake wa kulinda na kuendeleza mapinduzi, Rais Shein alimtunuku marehemu Nishani ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi mwaka 2014.