25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein aongoza hitma kumwombea Karume

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameongoza hitma ya kumwombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume, iliyofanyika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.

Hitma hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa SMZ, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd. 

Viongozi wengine waliohudhuria katika hitma hiyo ni  Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu.

Hitma ya kumwombea dua mzee Abeid Amani Karume, ambapo pia ni miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin pamoja na hitma iliyohitimishwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka Masjid Noor Muhammad.

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alitoa mawaidha na kumwelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Katika mawaidha hayo, Sheikh Soraga alisisitiza haja ya kuendeleza na kudumisha amani na utulivu uliopo ikiwa ni miongoni mwa misingi madhubuti iliyoachwa na muasisi wa Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.

“Yeye ndio mkombozi wetu kwani amefanya mambo mengi na sote tuko tayari  kushuhudia mema yote aliyoyafanya hapo siku ya kiama itakapofika mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W),”alisisitiza Sheikh Soraga.

Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika Aprili 7, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimwombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui.

Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Samia Suluhu Hassan, Mzee Hamad Ussi Haji aliyeweka shada la maua akiwawakilisha wazee wa CCM.

Mwisho

Ugatuaji wa madaraka utakuwa kisheria

Na Mwandishi Wetu

-Masasi 

SERIKALI imesema Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka ya mwaka 2019 ambayo hivi sasa ipo hatua ya rasimu, itakapokamilika itakuwa na nguvu ya kisheria na kisera tofauti na ile ya mwaka 1998.

Hayo yameelezwa juzi mjini Masasi mkoani Mtwara na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Edwin Mgendera baada ya kufungua kikao kazi cha kupokea maoni ya wadau juu ya rasimu ya sera ya Taifa ya ugatuaji wa madaraka ya mwaka 2019 kwa wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Alisema mafanikio na changamoto zilizotokana na utekelezaji wa Sera ya Ugatuaji ya mwaka 1998, imeiwezesha serikali kuja na sera ya jumla ya ugatuaji kitaifa ambayo itakuwa na nguvu za kisheria na namna bora ya kutekeleza na kutoa huduma kwa ufanisi kwa wananchi toka juu serikalini hadi ngazi za chini za kitongoji na mtaa halmashauri.

Alisema mwelekeo wa serikali kwa sasa, ni wa kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka ambayo itawekewa nguvu za kisheria na kisera ili kurahisisha suala la utoaji huduma kwa wananchi moja kwa moja kutoka serikali kuu hadi ngazi za kitongoji na mtaa.

 “Aidha Sheria Na. 7 ya Halmashauri za Wilaya ya mwaka 1982 (sura 287) na Sheria Na. 8 ya Halmashauri za Miji ya mwaka 1982 (sura 288) zinazipa mamlaka hizo majukumu ya kutoa huduma kwa jamii katika maeneo husika,” amefafanua bwana Mgendera. 

Aliitaja sheria ya Tawala za Mikoa ya Mwaka 1997 ambayo inazipa tawala za mikoa jukumu la kuratibu maendeleo katika Mikoa yao ikiwemo kuzisimamia na kuzisaidia mamlaka za Serikali za Mitaa katika kutoa huduma bora kwa usawa kwa jamii.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Kisekta kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Juma Idd alisema hivi sasa timu yake ipo  mikoa hiyo, baada ya kukamilisha kazi  mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa.

Alisema baada ya hapo timu yake, itakwenda mikoa ya mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma itashirikishwa, na baadaye zoezi hilo kuhamia mikoa ya kaskazini, magharibi na kanda ya ziwa.

Mwisho 

Wanafunzi waaswa kujitenga na makundi yasiyofaa

Na ALLAN VICENT

-TABORA

WANAFUNZI wa Shule za Msingi na Sekondari mkoani Tabora wametakiwa kujiepusha na makundi yasiyofaa ili waweze kuwa na maendeleo mazuri shuleni ikiwemo kufanya vizuri darasani. 

Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa mkoa huo, Aggrey Mwanri,  katika sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Huduma ya Mtoto hapa nchini inayosimamiwa na Shirika la Compassion International iliyofanyika katika kanisa la TAG-Kitete Christian Center mjini hapa.

Mwanri alisema kuwa mtoto anayesoma shule akianza tabia ya kuongozana na marafiki wabaya au kujihusisha na vitendo vibaya, asipokemewa au kuonywa mapema atabadilika kitabia na kuwa sawa na wenzake wenye tabia hiyo.

Alisema malezi mabaya ya watoto nyumbani hupelekea watoto walio wengi kujiingiza katika makundi yasiyofaa ikiwemo ngono, uvutaji bangi na udokozi  hivyo kushindwa kuendelea na masomo yao.

Alitaja athari za watoto hao kujiingiza katika makundi yasiyofaa kuwa ni kuolewa katika umri mdogo na kupata mimba za utotoni jambo ambalo huwafanya washindwe kufikia ndoto zao kielimu na kimaisha.

Alipongeza shirika hilo la Kimataifa kwa kulea vizuri na kusomesha watoto walio katika familia maskini kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu ambapo ilielezwa kuwa watoto zaidi ya 5000 wameingizwa katika huduma hiyo mkoani hapa.

“Wazazi tekelezeni wajibu wenu ipasavyo, kemeeni tabia zisizofaa kwa watoto wenu, msikae kimya, watoto wanaharibikia kwenu, ninyi ndio walezi wa kwanza kwa watoto wenu, toeni ushirikiano kwa shirika hili’,” alisema.

Naye Askofu wa Kanisa la Moravian mkoani Tabora, Mchungaji Ezekiel Yona alipongeza shirika hilo kwa moyo wao wa upendo ambao umewezesha watoto waliokuwa hawana matumaini ya kupata elimu kwenda shule na kupewa mahitaji yao yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles