-Azindua mpango wa makazi wa Watumishi Housing Investment
Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ametoa wito kwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, halmashauri na Wizara ya Ardhi kushirikiana kuhakikisha nyumba za watumishi wa umma zinajengwa karibu na maeneo yao ya kazi.
Akizungumza jijini Dodoma leo Desemba 11, 2024, wakati wa kuzindua Mpango wa Makazi kwa Watumishi wa Umma katika mradi wa nyumba za Watumishi Njedengwa unaomilikiwa na Taasisi ya Watumishi Housing Investment (WHI), Dk. Mpango amesema kuwa mtumishi anayefanya kazi mjini hapaswi kulazimika kuishi maeneo ya pembezoni mwa mji.
“Ninatambua changamoto ya upatikanaji wa nyumba. Ninashauri Ofisi ya Rais, halmashauri na wizara kulifanyia kazi suala hili ili nyumba zijengwe karibu na kazi na mahitaji ya msingi,” amesema Dk. Mpango.
Dk. Mpango amesema haiwezekani mtumishi afanye kazi kazi mjini lakini makazi yake yawe pembezoni mwa Mji hivyo ni lazima nyumba zao zijengwe jirani na maeneo yao ya kazi ili kurahisisha ufanyaji kazi zao.
“Kwanza ninatambua changamoto ya upatikanaji wa nyumba ninaushairi Ofisi ya Rais,Halmashauri na Wizara kulifanyia kazi suala hili ili ujenzi uwe karibu na kazi na mahitaji ya msingi,” amesema Dk. Mpango.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango ameagiza Wizara ya fedha kuharakisha mchakato wa Watumishi Housing Investments waweze kukopa ili kuweza kujiendesha.
Hatua hiyo imekuja kufuatia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kumweleza Makamu wa Rais kuwa wanatamani kupata mkopo ili waweze kujiendesha.
Makamu wa Rais amesema: “Ombi nimelisikia mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu ya fedha waharakishe mchakato waweze kukopa,” amesema Dk. Mpango.
Aidha Dk. Mpango amewapongeza Taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kazi nzuri waliyofanya kwa kuhakikisha wanafika maeneo ya vijijini.
“Ili Mpango huu ufanikiwe ni muhimu kuweka taratibu rafiki ili watumishi waweze kununua nyumba kwa kupitia mishahara.Ninapongeza sana katika kuwezesha malipo kwa njia rafiki kupitia malipo ya kila mwezi na hati miliki na kuwawezesha kiuchuki ili kuomba mikopo,” amesema Dk. Mpango.
Amesema mpango huo unalenga kupunguza changamoto hasa watumishi wa kawaida kukosa makazi bora na nafuu.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mifuko ya hifadhi ya Jamii na Sekta binafsi kuhakikisha nyumba zinapatikana kwa wingi hasa katika maeneo ya vijijini.
Hata hivyo, Dk Mpango amesema ili mpango ufikiwe malengo lazima kuwe na uwazi na uwajibikaji kwa kuwashirikisha wadau.
“Imani yangu kuwa ujenzi wa nyumba wilayani na vijijini utachochea sekta binafsi kuunga mkono jitihada hizi,” amesema Dk. Mpango.
Aidha, amewataka watumishi wa umma kuchangamkia fursa ya ununuzi wa nyumba hizo huku akiagiza wazitunze.
Dk. Mpango amesema Serikali itaendelea kuunga mkono kuhakikisha watumishi wanapata nyumba kwa bei nafuu.
Vilevile, Dk. Mpango ameagiza Watumishi Housing Investments kuangalia namna bora ya kuongeza ukubwa wa nyumba zao.
“Nimeingia kwenye nyumba ile ni nzuri lakini ni nyumba ya familia ndogo lazima tufikirie nyumba bora na kubwa. Mfano ana mtoto mmoja baadae labda akaongeza wawili ni muhimu wapewe maeneo ambayo akiwa mtumishi wa kawaida ataendelea kuona fahari na wageni wake,”amesema Dk. Mpango.
Pia ameagiza nyumba zinazojengwa ni muhimu kuzingatia ubora na thamani stahiki huku akikumbusha upandaji wa miti.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene mpango huo ulibuniwa serikalini miaka 10 iliyopita ambapo malengo kuwezesha upatikanaji wa makazi na kuwawezesha watumishi kupata umiliki wa nyumba.
Amesema Mpango huo ulibiniwa na Serikali mara baada ya watumishi wengi kushindwa kununua nyumba na masharti ya kukopa kuwa magumu na ya kibiashara.
“Nisisitize shida kubwa ya makazi hata kwa wale waliopo mjini ni kukosa makazi hasa wale wanaonza kazi,wanapaswa kukaa karibu na maeneo yao ya kazi,” amesema Waziri Simbachawene.
Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Investments, Dk. Fred Msemwa amesema wataendelea kupambana kuhakikisha watumishi wa Umma wanakuwa na nyumba bora.
Amesema wana ujenzi wa nyumba za aina tano na zimebuniwa kwa aina mbalimbali ambapo bei zinakuwa kutokana na ukubwa wa nyumba zikowemo zile za maghorofa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Watumishi Housing Investments, Badru Abdurazack, amesema wamejipanga kuongeza nyumba za bei nafuu ambapo makusudio yao ni kuanza kukopa fedha katika vyanzo mbalimbali ambapo kwa sasa hawana deni lolote.
Hata hivyo amesema bado wanakabiliwa na changamoto ya kuwa na mtaji mdogo hivyo wameiomba serikali waweze kukopa ambapo fedha zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.
Kwa upande wake Mkuu wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema wanajivunia kuona nyumba 209 ambazo zinazinduliwa kupitia WHI.