25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ndumbaro azindua mpango wa miaka 10 kuenzi urithi wa utamaduni

*Ni kueleka maadhimisho ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

Wizara ya Maliasili na Utalii imezindua mpango wa miaka 10 wa kuenzi urithi wa utamaduni ikiwa ni kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Aprili 13, mwaka huu.

Mpango huo una lengo la kuenzi na kusheherekea mchango wa Mwalimu Nyerere katika nyanja mbalimbali kitaifa na kimataifa.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na familia ya Mwalimu Nyerere ambayo iliyowakilishwa na Madaraka Nyerere na wawakilishi wa Wizara na Taasisi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Februari 3,2022 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro amesema mpango huo ni sehemu ya mpango wa miaka 10 wa kuenzi na kusherehekea urithi wa maisha ya mwalimu Nyerere.

Amesema mpango huo una lengo la kuwashirikisha wadau ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mchango wa mwalimu Nyerere Kitaifa na Kimataifa.

Lengo jingine ni kuandaa kutangaza kumuenzi mwalimu na umuhimu wa kukusanya , kuendeleza kuhifadhi na kutangaza rasilimali za urithi wa Mwalimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho ili kukuza na kuendeleza utalii.

Waziri Ndumbaro amesema maadhimisho ya miaka 100 ya mwalimu Nyerere (Mwl Nyerere @100 ni sehemu ya kutekeleza mpango wa miaka 10 wa kuenzi na kusherehekea urithi wa maisha ya mwalimu yanatarajiwa kufikia kilele Aprili 13,2022 Butiama mkoani Mara.

“Aprili 13, ndio siku aliyozaliwa Mwalimu Nyerere na kama angekuwa hai angetimiza miaka 100 lengo ni kuenzi na kusheherekea mchango wa mwalimu Nyerere katika nyanja mbalimbali kitaifa na kimataifa,” amesema Dk.Ndumbaro.

Ameongeza kuwa iwapo mpango huo utaweza kusimamiwa ipasavyo na kutekelezwa nchi itaweza kutangazwa kwa kazi zilizofanyika chini ya Mwalimu Nyerere, kutakuwa na makumbusho ya wapigania uhuru ya kwanza Afrika nakwamba urithi wa mwalimu utatambulika.

Amesema kuelekea kilele hicho, matukio mbalimbali yanatarajiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na mikutano ya wadau, mashindano ya baiskeli, matembezi ya hiari, ngoma za asili, Mwalimu Nyerere Marathon ambayo itafanyika kabla ya kilele Aprili 13,2022.

Waziri Ndumbaro amewatangazia wananchi kutengeneza nembo ambayo itatumiwa katika maadhimisho hayo na mshindi nembo yake itatumika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles