30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Mangula: Uimara wa CCM ni vikao na mazungumzo

Na Ramadhan Hassan, Kondoa

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula amesema uimara wa chama hicho ni pamoja na kufanya vikao na kuzungumza.

Akizungumza leo Februari 2,2022 katika Maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika Kimkoa katika kijiji cha Bumbuta wilayani Kondoa mkoani Dodoma, Mangula amewataka viongozi wa chama hicho kuwa na desturi ya kufanya vikao vya mara kwa mara ili kutatua matatizo ambayo yanawakabili Watanzania.

“Uimara wa CCM ni kuongea na kujadiliana hivyo ni lazima kupeana mawazo kipi cha kufanya. Wazee wangu mna baraza mkiona kuna jambo la ovyo kaeni, vijana, kina mama, wazazi kaeni kisha muisome Ilani ya CCM,”amesema Mangula.

Aidha, Mangula amewataka wana CCM kutochukulia kila ajenda ni kero huku akisisitiza umuhimu wa kufanyika kwa vikao vya shina kila mwezi vitakavyowasaidi kujua changamoto zilizopo.

Kuhusiana na miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, Makamu Mwenyekiti huyo amesema ni siku ya kufurahia kilichofanywa na chama hicho katika sekta mbalimbali.

“Tunaendelea kujivunia amani iliyopo,nchi imetulia tumesimamia misingi,” amesema.

Katikahatunyingine Mangula ametambua mchango wa viongozi mbalimbali walioshiriki kuleta maendeleo wilayani Kondoa pamoja na kuhakikisha CCM inafanya vizuri.

Amewataja baadhi ya viongozi hao kuwa ni Bakari Suru, Abdallah Mohammed Jumbe, Chuma Athuman Iluja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kondoa Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk, Ashantu Kijaji amesema jimbo hilo limekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya miaka 45 ya CCM.

“Mwaka 1977 kulikuwa kuna kituo kimoja cha afya leo tuna vituo saba na cha nane tumepokea fedha tunajenga Pahi. Mwaka 1977 mradi wa Ntomoko ulikuwa hautoi maji lakini leo una toa maji na tuna visima 81 na tumepata gari katika magari 26 ya kuchimba visima yaliyotolewa, hivyo tutapata gari moja tutachimba visima katika vijiji mpaka katika vitongoji,”amesema Dk. Kijaji.

Naye, Katibu wa CCM,Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga amesema wanalaani mauaji ya watu watano wa familia moja yalitokea hivi karibuni katika eneo la Zanka wilayani Bahi ambapo amedai kuna haja ya mabalozi kutambua wageni ambao wanaingia ili kuongeza usalama katika eneo husika.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa CCM, wilaya ya Kondoa, Mohammed Kova amesema kuna maendeleo ambayo yamepatikana katika miaka 45 ya kuzaliwa CCM ambapo amedai zamani kulikuwa hakuna shule na walikuwa wakienda Mpwapwa lakini kwa sasa katika kata 21 kuna shule 26.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles