Glory Mlay -Dar es salaam
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema asilimia 30 ya watoto hapa nchini wamedumaa huku asilimia tano ya watu wazima, hasa kina baba wakiwa na viribatumbo.
Hayo aliyasema jana Dar es Salaam wakati alipotembelea mabanda ya vyakula vya asili katika Tamasha la Utamaduni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Jamafest), linaloendelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Dk. Ndugulile alisema tatizo hilo linasababishwa na watu kutokujua kupika.
Alisema Watanzania wengi hawajui kupika kwani wanatumia mafuta mengi katika vyakula, wanakula vyakula vyenye sukari nyingi na kusababisha watoto wao kudumaa kutokana na kushindwa kupatiwa lishe inayostahili.
Dk. Ndugulile alisema mikoa ambayo inalima vyakuka vingi kama Mbeya na Songwe ndiyo inayoongoza kwa watoto kudumaa kutokana na kushindwa kupangilia chakula.
“Watanzania wengi hawajui kupika, hawajui jinsi ya kupangilia chakula, wao wanakula ili mradi kinafika tumboni, ndio maana wanaume wengi ambao wanakunywa pombe kupita kiasi wakikutana na vyakuka hivyo wanakuwa na viribatumbo na watoto kudumaa.
“Vyakula vingi vinatakiwa kupikwa kwa kuchemshwa na sio kujaza mafuta kama watu walivyozoea katika familia yako, pia utumiaji wa nazi nao unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la viribatumbo na udumavu kwa watoto,” alisema.
Alisema wizara hiyo ina mpango wa kupiga kambi katika mikoa hiyo ili kutoa elimu kuhusu lishe bora na jinsi ya kupangilia ulaji wa chakula katika familia zao.
Dk. Ndugulile alisema pia matatizo hayo yanaweza kuondoka endapo watu watazingatia lishe bora, kufanya mazoezi na kupunguza unywaji wa pombe kupita kiasi, hasa kwa wanaume.