Na Safina Sarwatt, Kilimanjaro
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi anatarajia kuwasili mkoani Kilimanjaro Juni 4, 2024 kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambapo atasikiliza kero za wananchi pamoja na kufanya mikutano ya hadhara.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Dk. Nchimbi ataambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa(NEC).
Akizugumza na wandishi wa habari katibu mwenezi CCM mkoa wa Kilimanjaro Ibrahim Urio amesema katibu mkuu anatarajiwa kuwasili Kilimanjaro Juni 4,2024, ambapo atapokelewa eneo KIA na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa pamoja na wananchi Wilaya ya Hai na kufanya mikutano wa hadhara eneo la Bomang’ombe.
Amesema katika ziara yake katibu mkuu CCM, Dk. Nchimbi pamoja na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) watasikiliza kero za wananchi pamoja mikutano ya hadhara.
Aidha, Urio amesema Juni 4,2024, atakuwa wilayani Hai na kuelekea Moshi mjini Juni 5, ambapo anatarajiwa kufanya kikao cha ndani na kufanya mkutano wa hadhara kwenye eneo la stendi kuu ya Moshi mjini.
“Juni 6,2024 atawasalimia wananchi wa eneo la Njia Panda ya Himo kabla ya kuelekea wilaya ya Mwanga na kufanya mikutano wa hadhara na kisha kuelekea wilaya ya Same Juni 7,2024, ambapo anatrajiwa kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi na kufanya mikutano wa hadhara na kwamba baada hapo antaondoka kuelekea mkoani Tanga,” amesema.