Na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, anatarajiwa kufungua Kongamano la Majeshi ya Nchi Kavu Afrika ya Mashariki.
Katika kongamano hilo zaidi ya wataalamu 300 wa masuala ya kijeshi na ulinzi watajadili changamoto zinazowakabili.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Kongamano hilo, Tracey Zurcher, ilisema kongamano hilo ambalo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndiye mwenyeji linatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 15 na 16, mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
“Nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki zina shauku kubwa ya kujilinda, sio tu kwa kuwa na maarifa bali pia kuwa na zana ili kuimarisha miundombinu ya ulinzi wao.
“Kutokana na misukosuko ya kisiasa wanayokumbana nayo sasa kwa upande wa uharamia na vikosi vya waasi, serikali hizi zinatakiwa kuongeza kwa kasi uwezo wa ulinzi wa nchi kavu pamoja na uwezo wa misaada ya kibinadamu,” alisema Zurcher.
Alisema kongamano hilo litaonyesha namna uwepo wa haja ya kuwa na ubora wa hali ya juu kimikakati na kiufundi kwa pamoja katika ngazi za kikanda.
“JWTZ inatazamia kununua zana, lakini pia tunajivunia kuyakaribisha majeshi na wawakilishi wa serikali kutoka nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi ambao wataelezea masuala muhimu kuhusu ulinzi kwa upande wa nchi kavu na majini pamoja na usalama kwa ujumla.
“Wataalamu wa masuala ya kijeshi kutoka nchi za Afrika ya Kusini, Malawi, Ethiopia, Msumbiji na Zambia pia wameelikwa,” alisema Zurcher.
Alisema kwa sasa Afrika Mashariki imekuwa eneo ambalo lina fursa kubwa katika sekta ya ulinzi.
Alisema hali hiyo inatokana na takwimu kuonyesha bajeti za ulinzi katika ukanda huu zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 13.6 kwa mwaka ambayo ni mara tano zaidi ya wastani wa sekta hiyo.
“Maoneo haya yatajumuisha wasambazaji zaidi ya 30 wanaongoza katika upande wa zana za kiulinzi ikiwamo Denel, Otokar na Armscor ambao wanaleta kampuni 10 za ulinzi na usalama kutoka Afrika ya Kusini kuonyesha ufumbuzi wao kwa upande wa Afrika Mashariki,” alisema Zurcher.
Jamani mbona the African na Rai hazimo katika mtandao? Fanyeni hima