Florence Sanawa, Mtwara
Naibu Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Dk. Mary Mwanjelwa amewataka wakuu wa wilaya zote zinazolima zao la korosho kuhakikisha wanadhibiti ulanguzi na kusimamia vizuri ugawaji wa pembejeo za korosho zinazotarajia kuanza kugawiwa Mei mwaka huu.
Amesema kumekuwapo na hujuma zinazofanyika kwenye zao la korosho hali inayotishia kuvuruga zao hilo la kimkakati kati ya mazao matano yanayotegemewa na serikali.
Akizungumza leo Aprili 24, wakati wa ziara yake mkoani hapa amesema pamoja na pembejeo kuwahi msimu huu serikali haitaruhusu ulanguzi wowote kufanyika kwenye uuzaji wa pembejeo ili wakulima wawahi kufanya maandalizi mapema.
“Serikali iko katika mikakati ya kuliwezesha zao la korosho linafanya vizuri hivyo wanaojaribu kufanya hujuma watashughulikiwa kwani tumedhamiria kupambana na wanaohujumu mazao yote,” amesema.
Aidha, Dk. Mwanjelwa amewaonya watakaoharibu na kuhujumu zao hilo kwa kuuza nje ya bei inayotakiwa hawataachwa salama kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Hamasisheni wakulima wajue kuwa hakuna pembejeo za bure bali wanapaswa kutunza fedha zao bei imepangwa na serikali hakuna ulanguzi wa aina yoyote utakaofanyika juu ya hilo kwa upande wa salfa na viuatilifu vingine,” amesema.