28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BOMBARDIER YAZUA MTIFUANO BUNGENI

Gabriel Mushi na Ramadhan Hassan – Dodoma


MJADALA wa ununuzi wa ndege mpya za Serikali zinazotumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), zikiwamo Bombardier Q400, umeendelea kuwagawa wabunge.

Baadhi ya wabunge wamedai Serikali imewekeza zaidi ya Sh trilioni moja kununua ndege hizo na hazitakuwa na faida, huku wengine wakiwapinga.

Pia wamesema kuna hatari ndege nyingine mbili za Serikali kukamatwa nje ya nchi baada ya ATCL kufunguliwa kesi ya madai ya zaidi ya Sh bilioni 80 London nchini Uingereza.

Mjadala huo wa ndege umeibuka bungeni mjini hapa wakati wabunge wakiendelea kuchangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino kwa mwaka 2018/19, iliyosomwa juzi na waziri Profesa Makame Mbarawa.

 

MDEE ACHAFUA HALI YA HEWA

Katika mjadala huo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema Serikali imetupa zaidi ya Sh trilioni moja kuwekeza katika shirika hilo.

“Nikiangalia randama ukurasa wa 11, mwaka huu wa fedha Serikali inatarajia kufanya ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya ATCL.

“Tutakumbuka mwaka jana Serikali kupitia Waziri wa Fedha, ilitenga bilioni zisizopungua 500 kwa ajili ya kununua ndege.

“Hoja si kupinga ununuzi wa ndege, hoja hapa ni fedha tunazowekeza ambazo ni matrilioni ya shilingi. Je, zinakwenda kuzalisha au tunakwenda kuzitupa na kupotea?

“Nina taarifa ya Msajili wa Hazina, anasema ameshindwa kufanya uchambuzi wa kina wa utendaji kazi wa ATCL  kutokana na kutokuwepo kwa taarifa za kutosha za kampuni.

“Kwa mfano, hesabu za kampuni zilizokamilika ni za mwaka 2014/15 tu, ambayo hata hivyo mahesabu hayo hayajatizamwa wala kupitishwa na bodi,” alisema.

Alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina ilishindwa kuchambua na kubainisha hali halisi ya uwekezaji ilivyo na hali ya ukwasi wa kampuni kutokuwa na mahesabu kwa muda mrefu.

“Ukija kwenye taarifa ya ATCL, wanasema shirika halikuwa na mpango wa biashara, yaani tunawekeza Sh bilioni 500 na sasa tunawezeka Sh bilioni 495, hivi unawekezaje wakati hakuna mpango wa biashara?

“Bunge, Januari walitoa taarifa za kamati na kuitwa wataalamu wa Serikali wanaosimamia mashirika na kusema shirika hili lina madeni ya Sh bilioni 317,” alisema.

Mdee alilitaka Bunge kutekeleza wajibu wake na lisijione liko salama, kwani ikigundulika fedha zimewekezwa kinyume na utaratibu kama nyaraka zinavyoonyesha, watachukuliwa hatua.

“Ni muhimu rais akajua hiyo kinga aliyonayo ya kikatiba inaangalia, kama kuna mambo aliyofanya makusudi kwa kuona hakuna usalama, mbele tutamshughulikia. Naongea kwa dhamira ya dhati, najua wabunge wengi wanajua,” alisema Mdee.

Baada ya kauli hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (CCM), waliibuka na kuomba kwa Spika Job Ndugai, kutoa taarifa na wengine kuhusu utaratibu.

 

MANYANYA

Naibu Waziri Manyanya alisema: “Kwanza Mdee achukulie kwamba rais wa nchi ni kiongozi anayeheshimika na watu wote, pili mambo yote yanayofanywa kwa nia njema yanatakiwa kuungwa mkono. Upinzani wenzetu wamekuwa wa kulalamika badala ya kutoa mawazo mbadala.

“Wabunge wa upinzani kipindi cha nyuma walikuwa wakichangia kuhusu ATCL na ndege zetu, wengine mmekuwa kama hamkumbuki. Siungi mkono michango ya kukashifu, na wote kukashifu tunaweza.”

 

LUKUVI

Kwa upande wake Lukuvi, alisema: “Nilitaka nikuombe kuhusu utaratibu nimsaidie Manyanya, kwamba tunachokisema kuhusu kanuni ya 64 inasema hivi; mbunge yeyote akiwa anazungumza hatatumia jina la rais kwa dhihaka katika mjadala au kwa madhumuni ya kutaka kulishawishi Bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani.

“Jina la rais halipaswi kutumika namna hiyo, neno kumshughulikia rais kwa maoni yangu halihusiani na mjadala huu. Mbunge aondoe maneno yake na kujielekeza katika mjadala.”

Baada ya maelezo hayo, Mdee alisema Rais alichaguliwa na Watanzania na Bunge ni wawakilishi wa Watanzania, hivyo lazima akosolewe na jina lake lazima litajwe kama anakwenda kinyume na utaratibu.

Alisema Bunge likiogopa kumtaja rais wakati wanapitisha bajeti na rais ni sehemu ya Bunge, wanalifanyia makosa taifa.

“Sijatumia jina la rais kwa kebehi. Nimesema tuna taarifa ya Msajili wa Hazina na ATCL zinazoeleza wazi,” alisema.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles