29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 7, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

DK. MWAKYEMBE ALIPOAMUA KUIDHALILISHA ELIMU YAKE

 “MIMI nawapa assignment wanitafutie ni msanii gani duniani amefanikiwa kwa kuimba masuala ya siasa” hakuishia hapo akaendelea kwa kusema “Hii ni entertainment industry sio political industry kama wanataka siasa waingie kwenye siasa wagombee udiwani, unataka kuimba kuhusu siasa wewe unaweza kuwa mwanasiasa wewe,” haya ni baadhi ya maneno yaliyotoka kinywani mwa msomi mwenye kiwango cha Phd (Shahada ya Uzamivu) Dk. Harrison Mwakyembe.

Huyu ni Waziri mwenye dhamana na masuala ya sanaa, ni fedheha sana kuwa na Waziri wa namna hii, Waziri wa Sanaa asiyejua kuwa fasihi simulizi ina kazi mbili yaani kuelimisha na kuburudisha lakini kama haitoshi Waziri huyu hana mifano ya wasanii waliofanikiwa kwa kuimba siasa, yaani Waziri huyu hamjui Bob Marley na nafikiri kamsahau Lucky Dube lakini yawezekana huko ni mbali vipi kuhusu marehemu Kapteni John Komba?

Lakini kule bungeni pia kuna wabunge wawili ambao ni Joseph Mbilinyi na Joseph Haule hawa ni wasanii na sehemu ya kazi zao ilitawaliwa na miziki ya siasa Je, hawatambui? Au huyu Waziri anaposema mafanikio anamaanisha kumiliki ndege au?

Eti watu wasiimbe siasa maana hamna watu waliofanikiwa kwa kuimba siasa, lakini si ninyi wazee mnasema kwamba miziki ya vijana haina tungo zenye mafunzo kazi yao wao ni kuimba mapenzi tu sasa mlitaka mafunzo ya aina gani? Au wasemwe wengine mkisemwa wanasiasa hamtaki?

Kama mtu akiimba kuwa Waziri Mwakyembe tulikulipa kodi zetu ukawe Mwenyekiti wa Kamati ya Richmond na hukutusomea ripoti yote ukafunika kombe mwanaharamu apite hayo hamtaki? Mnataka wasanii wote waimbe inama kidogo shika magoti, nimesimama nyuma kama ngongoti? Halafu jamii ikiharibika mnawarudishia lawama wasanii.

Tuliosoma fasihi tunafahamu vyema kuwa tabaka tawala huwa halipendi kunyooshewa kidole ndio maana tuliambiwa uhuru wa Mwandishi upo endapo tu atashindwa kulidhuru tabaka tawala ndio maana sishangai leo hii kumuona mjomba Mpoto kuwa karibu na wakubwa na hata salamu zake hazitumi tena kwa mjomba, siku hizi yeye na Sizonje damdam.

Leo tumefikia hatua ya kuambiana miziki ya kuimba nafikiri ipo siku kuna mwanasiasa atasema watu wasisome sana maana duniani hamna tajiri profesa hata hapa Tanzania hawa kina Bakhresa hawana Phd kama Dk. Mwakyembe lakini wana hela nyingi.

Kabla hatujawakataza kuimba siasa hebu tujiulize ni kwanini wanaimba kuhusu siasa? Watu wanaimba kuhusu siasa kwa sababu dunia inaendeshwa na siasa, leo machafuko ya Syria ni matokeo ya siasa, vipi kuhusu Libya na Iraq?

Bila siasa leo wangekuwa pale? Lakini tuachane na nchi za watu hata umasikini tulionao Tanzania ni matokeo ya siasa na wanasiasa uchwara ambao hawaishi kutulaghai, watu tuna rasilimali za kila aina lakini bado wananchi ni masikini wa kutupwa halafu unatuhamasisha tuimbe ‘Baby I Love you’ wakati kuna mama zetu wanatembea umbali mrefu kutafuta maji na wajawazito wengi hufariki kwa kukosa huduma nzuri za afya?

Wasanii ni sauti ya jamii, hii ina maana wanatakiwa kutusemea pale ambapo wengi wetu tunashindwa kusema, nchi yetu ina matatizo kila idara hivyo nilidhani wanasiasa wanahitaji watu wa kuwakumbusha wajibu wao.

Nchi ambayo hospitali hazina dawa, wagonjwa wanalala chini, rundo la watumishi hewa na vyeti feki, rushwa kila sekta wasanii wake wanaachaje kuimba kuhusu siasa?

Jambo moja ambalo nalifahamu vyema ni kuwa ukweli unauma, kwa hiyo wanasiasa kama hamuupendi basi timizeni majukumu yenu kama mnavyoahidi majukwaani vinginevyo mtaendelea kusikia nyimbo lukuki zenye maudhui ya kisiasa.

La mwisho Dk. Mwakyembe unajidhalilisha sana na si wewe tu unaitia doa hata elimu yako, kitendo cha kusahau kuwa kazi ya fasihi si kuburudisha peke yake jambo ambalo hata mtoto wa Sekondari anafahamu hivyo ni unajiaibisha.

Alianza Prof. Lipumba kuidhalilisha taaluma yake sasa naona unafuatia ila chonde chonde tunawaomba mzitetee elimu zenu maana kwa ujenzi huu wa hoja ipo siku watoto wetu watakataa kusoma wanaposikia hoja za Daktari zinafanana na mtoto wa shule ya msingi, chondechonde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles