27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KENYA  AGOSTI 2017: SIASA ZA JUBILEE, NASA VINAVYOSAMBARATISHA WANANDOA

JOSEPH HIZA Na Mashirika ya Habari


TOFAUTI na chaguzi zilizopita ambako kulikuwa na sehemu kubwa ya Wakenya, wasiofurahia siasa, safari hii hali inaonekana kubadilika.

Pengine ni kutokana na ugatuzi, uongozi dhaifu, gharama kubwa za maisha zinazoshuhudia bei kubwa ya chakula, rushwa kwa kutaja machache, raia wengi wanaonekana kuzama katika siasa kuliko kipindi chochote kile.

Wakati homa ya uchaguzi huo ikizidi kupanda kuelekea Agosti 8 mwaka huu, baadhi ya athari zinazotokana na homa hiyo zimeshajitokeza zikivuka mpaka kutoka uhasama wa kisiasa hadi kijamii.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wafuatiliaji wa siasa nchini humo, uhasama si tu unasababisha uadui baina ya wageni na marafiki katika mitandao ya jamii na makundi ya WhatsApp groups, bali pia majumbani na makazini.

Kuna ndoa ambazo tayari zinayumba au zimevunjika kutokana na kushabikia pande tofauti baina ya vyama vya Jubilee chini ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto na muungano wa upinzani wa NASA.

NASA ambayo mbali ya mgombea wake wa urais Raila Odinga na mwenza wake Kalonzo Musyoka, ina vinara wengine kama vile Musalia Mudavadi na Moses Wetangula kutoka jamii ya Luhya.

Wakati Uhuru na Ruto wakitokea makabila makubwa ya Kikuyu na Kalenjini, Raila na Kalonzo wanatokea Luo na Kamba.

Kwa msingi huo athari za uhasama huo zimeingia katika ndoa pale ambapo wenzi wametokea kambi hasimu kisiasa.

 “Katika nyumba yangu, wakati wa taarifa za habari hali huwa mbaya sana. Wakati habari kuhusu Nasa inapovuma, mke wangu hulazimisha stesheni ibadilishwe kwa sababu anaiunga mkono Jubilee na anamchukia Raila kwa sana,”analalamika James, kutoka kabila la Luhya, ambapo mkewe ni Mkikuyu.

James anasema hali inakuwa mbaya sana wakati anapoeleza namna nchi inavyoongozwa vibaya na utawala wa chama cha Jubilee.

Hata hivyo, kutokana na kupanda mno kwa gharama za maisha ambazo zinaleta maumivu katika bajeti ya familia, mkewe ambaye pia anaonja joto la makali ya maisha, wakati mwingine anakubaliana naye.

Lakini kwa sababu ya kabila lake na kauli zinazoiandama Jubilee na ukabila, hisia zake kila wanapozusha mjadala huo, humweka katika wakati mgumu.

“Hata malalamiko dhidi ya Jubilee yanachukuliwa kama mashambulizi binafsi. Unapoishambulia Jubilee ni kama unamshambulia yeye, anakasirika, ananichunia na hata kulipa kisasi kwa kuninyima haki ya ndoa,”analalamika.

Baadhi ya Wakenya katika mitaa ya Nairobi wamekiri kupiga marufuku siasa katika nyumba zao ili kuzilinda ndoa zao huku wengine wenye kuweka ubinafsi wakipiga marufuku tu kuzungumzia kambi hasimu.

Lakini kuna ambao wameacha kuzungumza kwa wanafamilia au marafiki wa karibu, kwa sababu tu ya uhasama huo baina ya Jubilee na Nasa.

“Mivutano haijaishia katika mitandao ya jamii, mitaani, mazishini, bungeni au katika mijadala ya televisheni kama watu wanavyodhani.”

“Katika baadhi ya nyumba zetu, huwezi kuzungumza siasa kwa sababu baadhi ya wanafamilia wataanza kujisikia vibaya’,” anasema Edwin.

Anatolea mfano wa ndugu yake mmoja, ambaye kwa sasa ametengwa kwa sababu anafanya kazi na Jubilee, pamoja na kwamba yu kabila la Luo.

“Anahesabiwa kama msaliti na watu wanamsusa,”anasema.

Hali mbaya zaidi kitandani hasa wenzi wanapokuwa wanatokea jamii hasimu ambazo zimeegemea zaidi Nasa au Jubilee.

Kuna mifano ya marafiki makazini kugeuka maadui kutokana na uhasama huu na wengine kuunda kambi hasimu kwa ajili ya Jubilee na Nasa. “Makundi mengi ya WhatsApp yamegeuka kuwa majukwaa ya vyama hivyo viwili.

Maadili na taaluma kama uandishi wa habari vimewekwa pembeni wakati wa mazungumzo yanapogusia kumuunga mkono Raila au Uhuru,”anafichua Rose, ambaye ni mwandishi wa habari.

Rose anasema kinachozungumzwa katika kundi la WhatsApp kazini daima huegemea mirengo ya kisiasa kuliko kitaaluma.

Katika moja ya kesi zilizoripotiwa hivi karibuni mwanamke katika eneo la Githurai mjini Nairobi alitishia kuvunja ndoa yake kwa sababu ushabiki uliopitiliza wa mumewe kwa mgombea urais wa Nasa, Raila Odinga huku akimchukia vikali Rais Uhuru Kenyatta.

Kali zaidi ni tukio la mume mwenye hasira kupiga marufuku habari kuhusu Uhuru na Ruto kusikika katika makazi yake!

Katika kuonesha uaminifu kwa Uhuru, mke ambaye anatoka Katikati ya Kenya wanakotokea Wakikuyu, ameamua kuachana na mumewe.

Mumewe huyo si tu humtukana Rais Kenyatta mara kwa mara rais bali pia hubadili kipindi cha televisheni kila mara Uhuru au naibu wake William Ruto wanapoibuka.

“Amepanga kuondoka na watoto kwa sababu amechoka na vitendo vya mumewe kumdhalilisha, kumlaani na kumtukana Rais na naibu wake kila wanapoonekana katika televisheni ilihali akijua anaumiza hisia za mkewe,”anafichua Diana, msaidizi wa wenzi hao.

Msichana huyo wa kazi alisema mke aliyeghadhibishwa na mumewe alitambulika kama Njeri, amekuwa akilalamika kuchoshwa na mumewe, ambaye jina lake la ukoo anajulikana kama Okoth akimuita Rais na kabila lake zima la Kikuyu majina mabaya na machafu.

Awali Okoth alikuwa akionesha uvumilivu kwa rais na naibu wake kila walipochomoza katika televisheni kwa angalau kuzomea, dhihaki na kuwaponda kwa kuashiria mkono kivivu.

Lakini mambo yalianza kubadilika kuwa mabaya hasa Serikali ilipokuwa ikishambulia upinzani, kitu kilichomfanya mume aanze tabia ya kubadili stesheni.

“Kila arudipo nyumbani akiwa amelewa, kamwe hafichi hisia zake za chuki kwa Uhuru na Ruto.

Hutoa kauli chafu kuwahusu wakati wa taarifa za habari akiwaita Tom na Jerry (vikatuni maarufu katika televisheni) ambavyo huwa hana muda navyo kabla ya kubadili stesheni,” alisema msichana huyo wa kazi.

“Sitaki kuona Tom na Jerry, badili stesheni mara moja,”mwanamume huyo daima hubwatuka kwa ukali.

“Hata hivyo kinachomuumiza zaidi mkewe ni kuwa hulilaani hadi kulitusi kabila zima la rais akiwaita wezi, akirejea uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na 2013,”aliongeza msichana huyo.

Kituko cha karibuni zaidi kilitokea wakati Rais akihutubia katika televisheni.

Mke anaripotiwa kumuomba mumewe amruhusu na familia kufuatilia kinachojiri katika hotuba ya rais, lakini alimkatalia.

Kutokana na mumewe kugeuka shabiki la kutupwa la Odinga, mke ameapa kukosa uvumilivu tena na kwamba ni wakati wa kufungasha na kuondoka.

“Kila mume anapokuwa nyumbani na marafiki zake, nyumba hugeuka uwanja wa siasa, huku mume akizungumza siasa mwanzo mwisho akiimba Jubilee iliiba kura katika uchaguzi wa 2013 na imepanga kufanya hivyo 2017. Habari kuhusu Rais zimepigwa marufuku kabisa nyumbani.

Hilo limemkosesha mwanamke furaha kila mumewe anapoizungumnza vibaya jamii yake ya Kikuyu,”anasema Diana.

Siasa kuelekea uchaguzi mkuu duniani kote ni suala linalobeba hisia kali na wataalamu wa saikolojia huonya wenzi kukaa nazo mbali baina yao.

Liliwahi kutokea kwenye ndoa yenye umri wa miaka 22 wakati wa uchaguzi wenye ushindani mkali nchini Marekani ulioshuhudia Donald Trump akichaguliwa kuwa rais.

Mwanamke ambaye ni mfuasi mkubwa wa Hillary Clinton alihitimisha ndoa yake hiyo yenye umri wa zaidi ya miongo miwili kutokana na mumewe kuwa mfuasi wa Trump.

Gayle McCormick (73) askari jela mstaafu mjini Washington, ambaye alijieleza kuwa mwanademokrasia mwenye mwelekeo wa kisoshalisti,” alisema aliamua kuvunja ndoa yake yenye umri huo baada ya mumewe kutangaza katika chakula cha mchana na marafiki kuwa alipanga kumpigia kura Trump.

Anasema kauli hiyo ilikuwa ya ‘kuvunja mkataba’, nilishtushwa,” aliviambia vyombo vya habari.

Ndoa au husiano zilizotetereka au kufa nchini humo zilikuwa nyingi ikichangiwa na ushabiki wa kambi za Trump na Clinton.

Nchini Kenya badhi ya wanandoa hulazimika kuumia kimya kimya kwa kutopanua sauti zao huku wengine wakijifanya kuunga mkono vyama vya waume zao.

"Katika hii nyumba kila mtu ni Jubilee, hayo mambo ya Nasa sitaki kusikia hapa," baadhi ya wanaume huunguruma wakiwalazimisha wake na watoto wao kuunga mkono vyama wanavyovishabikia.

Kwa sasa nchini humo wanawake kutoka Nasa na Jubilee huogopa kuingia uhusiano kutoka kwa wanaume kutokea upande hasimu tofauti na wanaume ambao huwajali kujaribu kuanzisha uhusiano kutoka kambi hasimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles