27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dk. Mpango: Masoko ya mitaji yaimarishwe

Na ANDREW MSECHU – Dar es Salaam


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuboresha mpango kazi wake wa kutoa elimu kwa umma na huduma zaidi kwa makundi yote ya jamii ili kuendeleza masoko ya mitaji kwa watu walioko vijijini.

Akizungumza jijini hapa juzi wakati wa kuwakabidhi vyeti wanafunzi 80 wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu waliofanya vizuri katika shindano la insha kuhusu masoko ya mitaji, alisema anaamini weledi na ujuzi waliopata wahitimu hao ni wa hali ya juu na utaleta kiwango cha ushindani wa kimataifa katika utendaji katika sekta ya masoko ya mitaji hapa nchini.

Alisema Serikali kupitia CMSA ina jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza sekta ya masoko ya mitaji ili kupata mitaji ya muda mrefu kwa kampuni na husaidia umilikishaji wa njia za uchumi kwa umma na kusaidia kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukuaji wa uchumi.

“Tunahitaji uwepo wa wataalamu wa kutosha wenye weledi wa hali ya juu katika masoko ya mitaji. Tukiwa na wataalamu wazalendo na waliobobea watasaidia katika kuhakikisha masilahi ya taifa yanalindwa. Hivyo ni imani yangu kuwa ninyi mliotunukiwa vyetu mtatoa mchango mkubwa kufanikisha azma ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda,” alisema.

Pia alisema Serikali inathamini na inatambua juhudi zinazofanywa kuongeza uelewa wa masoko ya mitaji na kuwawezesha wananchi kiuchumi na kijamii.

Alisema wanafunzi hao 80 waliofanya vizuri katika wanafunzi 15,004 walioshiriki shindano hilo ni sawa na asilimia 0.4 tu ya walioshiriki, hivyo ipo haja ya kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi kubwa zaidi ya wanufaika kutokana na uhaba wa watendaji katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama alisema wamekuwa wakishirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) kuandaa mpango wa kuwawezesha washiriki wa shindano hilo kuwa wawekezaji halisi.

Alisema wanatarajia mafunzo hayo yatasaidia kujenga ujuzi wa washiriki katika masoko baada ya kupata uzoefu kutoka Mauritius.

“Tayari baadhi yao wameanzisha kampuni zilizo katika mchakato wa kupata leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji. Mojawawapo ni Beacon Financial Services ambayo mkurugenzi wake ni mwanafunzi aliyepo hapa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles