26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk.Mpango, balozi wa Italia wateta Ikulu

Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango hii leo agosti 21, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Italia hapa nchini Marco Lambardi, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemhakikishia balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi kama vile madini, misitu na mifugo hivyo ni Taifa lenye utajiri wa malighafi zinazorahisisha katika uanzishaji wa viwanda.

Aidha Dk. Mpango amesema serikali ya Tanzania inatambua mchango wa Italia katika kuendeleza elimu ya ufundi hapa nchini na kuwasisitiza kuendelea kuwekeza zaidi katika elimu hiyo.

Kwa kutambua kwamba Italia ni mwenyekiti mwenza wa mkutano mkuu wa mazingira wa umoja wa mataifa utakaofanyika mjini Glasgow, Makamu Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua zote za kulinda mazingira na kufanya uhifadhi ikiwemo kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji hivyo ni vema mataifa yalioendelea kutambua mchango wa uhifadhi ambao umefanywa na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi hizo.

Kwa upande wake balozi Lambardi amesema Italia na Tanzania zimekua na ushirikiano wa muda mrefu na hivyo wataendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Amesema tayari wanafanya makubaliano ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar ili kuendelea kukuza sekta ya utalii hapa nchini.

Aidha amesema wameonesha nia ya kutoa mchango katika sekta ya afya nchini na ifikapo Septemba mwaka huu, ujumbe kutoka Italia utafika kukutana na uongozi wa Wizara ya Afya ili kubaini mahitaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles