Gabriel Mushi, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Serikali kwa mwaka 2017/18 ni Sh bilioni 156.1 sawa na asilimia 38 ambazo ametaka zielekezwe kwenye matumizi sahihi zisitumiwe vibaya na ‘mchwa’.
Dk. Mpango amelazimika kutoa ufafanuzi huo leo bungeni jijini Dodoma baada ya kuibuka mkanganyiko kuhusu takwimu za fedha hizo wakati Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiwasilisha hotuba yake.
Akiwasilisha hotuba hiyo, Kamwelwe amesema kutokana na uhaba wa fedha hadi kufikia Machi mwaka huu fedha za miradi ya maendeleo zilizopokelewa ni Sh bilioni 347.5 sawa na asilimia 56 na Sh bilioni 12 sawa na asilimia 52.45 ya fedha za matumizi ya kawaida zilitolewa.
Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa alisema fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa kwa mwaka 2017/18 ni Sh bilioni 135 sawa na asilimia 22.
Takwimu hizo zilionekana kupingana na zilizotolewa na Waziri Kamwele hali iliyosababisha baadhi ya wabunge kueleza kutoridhishwa na mkanganyiko huo.