25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mollel ayataka mashirika kujikita kutafuta suluhu kwa wagonjwa

Na Clara Matimo, Mwanza

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, ameonyesha kutopendezwa na baadhi ya mashirika na taasisi zinazojishughulisha kutoa huduma za afya kutumia fedha wanazopewa na wafadhili kufanya semina, warsha na makongamano badala ya kutafuta suluhu kwa magonjwa yanayowasibu walengwa.

Ameyataka mashirika hayo kuiga mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan, alivyotumia fedha Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani(IMF) ili kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii ambazo zinatoa suluhisho la changamoto zinazomgusa kila mtanzania hata anayeishi kijijini.

Baadhi ya wadau wa sekta ya afya wakiwa kwenye mkutano na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel,(hayupo pichani) uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekoutoure.

Dk. Mollel ametoa kauli hiyo leo Julai 4, mwaka huu wakati akizungumza na wadau hao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekoutoure  akiwa kwenye ziara  ya kuzunguka mikoa ya kanda ya ziwa kukutana nao pamoja na viongozi wa sekta ya afya  lengo likiwa ni kuweka mipango  itakayowezesha  kufanya shughuli kwa pamojakatika utekelezaji wa mwaka mpya wa fedha ulioanza Julai Mosi, 2022  ili kutatua changamoto za masuala ya afya kwa walengwa.

Amesema kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya taasisi na mashirika hayo kushindwa kutekeleza malengo ya fedha hizo badala yake huwezesha watu kuhudhuria semina kwa lengo la kubadili mitazamo ya jamii jambo ambalo halina tija wala halitoi suluhu kwa wagonjwa wakati  wafadhili hutoa  fedha zao wakijua zinakuja kuwashibisha wenye njaa lakini kuwanufaisha wenye shibe.

“Tumechoka warsha semina, capacity building kila tukipima hakuna mabadiliko sijasema watu wasifanye attitude  ila zipungue kwa asilinia 70 hizo fedha zielekezwe kwenye vitendo  isije ikaishi tu kwenye safari, na vikao, huwezi kuchenji attitude(mtazamo) lakini mgonjwa akafa ni bora umpe chakula ili apone fedha za wafadhili zisitumike asilimia kubwa kulipana posho kama ulikuwa unakaa vikao 50 kwa mwezi punguza vibaki 20 ili fedha  nyingi zitumike kwa walengwa.

 “Serikali inatambua wadau mnafanya  vitu vingi ambavyo vinagusa jamii na kuleta impact kwenye uchumi wetu wa leo na baadaye lakini tambueni kwamba karibia nusu ya vifo vya watoto vinatokana na kuzaliwa njiti, ukosefu wa lishe wakati mnapambana na attitude  wanazaliwa watoto njiti 100  ni vizuri ukawapa vifaa vya kuwasaidia kukabiliana na hali hiyo  wakati ukiendelea  na  attitude  tupambane kusaidia kuokoa maisha,”amesema na kuongeza .

“Tulikuwa tunaadhimisha siku ya mabusha wamewaleta wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakurugenzai aliyeandaa maadhimisho anaeleza changamoto za wenye mabusha kuwa ni gharama za upasuajia Sh 270,000 nilitarajia wawalipe madaktari na wauguzi wapite kwenye vituo vya afya wawafuate wagonjwa wawafanyie upasuaji halafu ndiyo  waniite naibu waziri au waziri wangu tuwape pole wagonjwa wakiwa wodini tunauwezo wa kuboresha na kuondoa changamoto za watanzania tukitumia resources zetu wenyewe na wadau,vitendo vinaongea kuliko maneno ukimwambia mtu compassion(huruma) kuliko attitude,” amesema.

Nao baadhi  ya wadau hao akiwemo, John Fulli, kutoka shirika la Americares  ambaye ni Mkurugenzi wa mradi wa USAID uzazi staha na Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Icap, Dk. John Kahemele, walisema ushauri na maelekezo ya Dk. Mollel  yana tija wako tayari kutekeleza  kwa kuboresha zaidi  katika ngazi ya utekelezaji wa miradi.

“Hakuna mtu ambaye atakataa jambo hilo la msingi alilolizungumza naibu waziri, uzuri amelizungumza tukiwa na watendaji wa serikali kwa sababu haya ni mambo ambayo pia huwa tunajadiliana  tunakuwa na mipango ya pamoja  ambayo tunafanya na serikali za mikoa na wilaya,  amesisitiza fedha zisiishie kwenye kulipana posho na safari  kwa hiyo itakuwa ni jambo zuri hasa tunapoanza mwaka mpya wa fedha ushauri na maelekezo aliyoyatoa  tutayazingatia.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuifungua Tanzania na kuifanya  iwe mahalia ambapo watu wanapenda kufanya nayo kazi amatengeneza mazingira ya miradi kama ambayo tunaitekeleza  kwa sababu huwezi ukapata ushirikiano wa mashirika ya nje kama mazingira yako ya ndani hayajakaa sawa, tunaahidi kufuata nyayo zake alizotuongoza kama alivyofanya kwenye matumizi ya Sh trilioni 1.3,”alisema  Dk. Kahemele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles