NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Sellasie Mayunga amesema kati ya viwanja 1,816,009, vilivyopimwa kati ya hivyo vyenye hati ni 586,000 tu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es salaam jana kabla ya makabidhiano ya ofisi ya Naibu Katibu Mkuu mpya, Dk. Moses Kusiluka ambaye hata hivyo hakuhudhuria makabidhiano hayo, Dk. Mayunga alisema ufinyu wa bajeti katika wizara hiyo, unachangia kuzorota kwa baadhi ya kazi, ingawa kuna baadhi ya changamoto zimeanza kutatuliwa.
Kuhusu baadhi ya watendaji wa wizara hiyo ambao wamekuwa wakilalamikiwa kutokana na utovu wa nidhamu na maadili kazini, wamechukuliwa hatua kwa kuwahamishiwa sehemu mbalimbali.
“Changangamoto tuliyokuwa nayo, ni ufinyu wa bajeti zimeanza kutatuliwa…kuhusu watumishi wenye utovu wa nidhamu ambao wanakuwa na tabia ya kuomba rushwa wamechukuliwa hatua.
“Yale majipu madogo madogo tulishayatumbua, kwa Serikali hii ya awamu ya tano, majipu yote yatatumbuliwa hapa hapa,wasitegemee kuhamishiwa popote,” alisema Dk.Mayunga.
Alimtaka Dk. Kusiluka kuhakikisha anashughulikia mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi uliopo Ziwa Nyasa ambao ulianza Mei 3,1967 hadi sasa haujapata ufumbuzi.