29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli: Msituadhibu

Pg 2*Asema kitanda chenye kunguni hakichomwi moto

*Ataka wananchi waichague CCM, aahidi kushughulikia ‘mchwa’

 

Bakari Kimwanga na Raphael Okello, Bunda

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amewaangukia wananchi na kuwaomba wasikiadhibu chama chake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

Mgombea huyo amewaomba wananchi kuichagua CCM na kuahidi kuwashughulikia watu ambao amewaita kuwa ni mchwa, endapo watampa ridhaa.

Akihutubia mamia ya wananchi wa mji wa Bunda mkoani Mara jana, Dk. Magufuli alisema amejipanga vizuri kuwateketeza mchwa hao mara tu baada ya kuingia madarakani.

“Nawaoamba wananchi msiiadhibu CCM, kwa kuwa nimejipanga kuwashughulikia mchwa serikalini.

“Nawaomba wana Bunda msiipe CCM adhabu…kama ambavyo huwezi kuchoma kitanda kinachoingiliwa na kunguni, badala yake utachoma kunguni, acheni tuwachome kunguni  walioko serikalini,” alisema Magufuli.

Kuhusu suala la kuwapatia wananchi wa Bunda maji, Dk. Magufuli alisema.

“Niwaahidi wanabunda,  mtapata maji ndani ya miezi mitatu tangu kuunda baraza langu la mawaziri… kama waziri  wa maji atashindwa kutekeleza ahadi hii, waziri huyo atageuka kuwa  maji,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi.

Alisema kila sehemu ambayo amekuwa akipita, amekuwa na kazi ya kuwaombea msamaha wagombea ubunge na udiwani na kuwasihi wananchi wawachague ili kama akiingia madarakani wasaidie kuleta maendeleo.

AMANI

Katika hatua nyingine Dk. Magufuli amepuuza hoja za baadhi ya watu wanaodai ametoa kauli za vitisho kwa wananchi kwa kuhusisha uchaguzi na vurugu za nchi ya Libya.

Akiwa katika Wilaya za Butiama, Bunda na Serengeti, kwa nyakati tofauti, Dk. Magufuli, alisema kamwe  hataacha kuzungumzia amani japo kuna watu wanachukizwa na kauli yake.

Alisema ataendelea kuhubiri amani ya nchi, kwani asipofanya hivyo ni bora asichaguliwe kuwa rais wa awamu ya tano.

“Nimeanzia Butiama kutokana na historia ya amani ya nchi hii. Najua wapo watu eti wanasema nisihubiri amani ya nchi…nasema  nitaendelea kuisemea wakati wote.

“Iwe usiku, mchana na hata wakati wote nitazungumzia amani, nisipohubiri amani basi sisitahili kuwa rais.

“…leo Mama Maria Nyerere yupo nchini Namibia anapokea tuzo ya amani  kwa sababu ya amani ya nchi yetu kutokana na misingi imara iliyowekwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC) pamoja na wasomi mbalimbali, kumtaka mgombea huyo kuacha kutumia mifano ya nchi za Libya na Misri katika kampeni zake.

Itakumbukwa katika nchi hizo, machafuko yalisababisha Kiongozi wa Libya, Kanali Muamar Gaddafi kung’olewa madarakani, huku nguvu ya umma nayo ikimuondoa madarakani Rais wa Misri, Hosni Mubarak.

Dk. Magufuli alisema amedhamiria kuwatumikia Watanzania kwa vitendo na atahakikisha anaunda baraza la mawaziri dogo, lakini lenye uadilifu.

 

JAJI WARIOBA

 

Naye Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba, jana aliibuka kwenye kampeni za Dk. Magufuli na kuwashangaza watu wanaobeza maendeleo yaliyopatikana  katika miaka 54 ya uhuru.

Jaji Warioba, alitoa kauli hiyo kwenye uwanja wa Mwenge kijijini Butiama alipopewa nafasi ya kusalimia.

Alisema umefika wakati watu wanaomtumia kama dira Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika kampeni zao wajitafakari zaidi.

Bila kutaja jina la mtu, Jaji Warioba alisema wakati wa mchakato wa urais ndani ya CCM kila mgombea alikwenda katika kaburi la Mwalimu Nyerere aliyezikwa eneo la  Mwitongo na kuanza mikakati yake.

“Wengine katika kampeni zao wanatumia maneno ya Mwalimu kama wamechanganyikiwa. Huwezi kumtumia Mwalimu Nyerere kama dira halafu unasema CCM haijafanya kitu, aliijenga Tanzania kwenye misingi na wote waliomfuata wanapita kwenye misingi yake,” alisema Jaji Warioba.

Alisema hatua ya nchi kupoteza maadili ilitokana na  uamuzi wa baadhi ya viongozi kuwa na uhusiano na matajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles