24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watake wasitake Ikulu tunaingia – Lowassa

0D6A1147NA MAREGESI PAUL, KONGWA

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema ana uhakika wa kuingia Ikulu kwa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wanaomkosoa wawe wanajibu hoja kwa kuwa yeye ana utaratibu wa kuwaeleza Watanzania atawafanyia nini baada ya kuingia madarakani.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

“Naomba nitofautiane na Tundu Lissu ambaye amesema hapa, kwa kusema ni lazima tuiondoe CCM madarakani kwa sababu hali yetu ni shwari kabisa.

“Nawatahadharisha waache, watu hao waache kusema uongo na kuwapotosha wananchi kwani matusi hayasaidii chochote.

“Nawaomba wajibu hoja za mendeleo, wao wanapiga maneno ya uongo kwa sababu ya kitu wanachotaka kukifanya.

“Kwa mfano, tumesema katika ilani yetu tutahakiki mikopo ya nje kwani hapa Sumaye amesema kila Mtanzania ana mzigo wa mkopo wa nje wa shilingi laki nane.

“Kwahiyo, hapa tunataka kujua hizo shilingi laki nane wanazodaiwa Watanzania zilitumikaje ili zisije zikawa zilitumika kuzungukazunguka duniani.

“Nawaambia waache kupiga kelele nyingi, watutayarishie maelezo tu, maana lazima Ikulu tutaingia watake wasitake. Tutakapoingia tutawataka vilevile wajibu hoja ikiwa ni pamoja na hili soko lenu la Kibaigwa limefikia wapi,” alisema Lowassa.

Pamoja na hayo, alisema atakapoingia madarakani, Serikali yake itatekeleza ahadi zote zilizoahidiwa huku ikiwaletea maendeleo ya kasi Watanzania wote.

“Nchi yetu toka mwaka 1961 haijaondokana na umasikini na badala yake umasikini unaongezeka kila siku. Kwahiyo sisi tutahakikisha kila mtu anaishi maisha bora, na kama alikuwa akila mlo mmoja, ale milo mitatu, kama alikuwa ana gari moja, awe na magari mawili, kama alikuwa na baiskeli moja, awe na pikipiki, kama alikuwa anavaa kanga mbili, avae tano.

“Tunataka maisha ya Mtanzania yawe ni ya mtu anayejiamini zaidi, na tutamwezesha ajitegemee zaidi kwani kuna watu wametudanganya kwa miaka mingi na wanafikiri umasikini ndiyo uongozi.

“Wanafikiri ukiwa kiongozi umasikini ndiyo unafaa, wanawadanganya, huo ni uongo ndiyo maana mimi nauchukia umasikini na hakuna mtu anayependa umasikini duniani.

“Naomba ruksa ya kwenda Ikulu nikawaonyeshe Watanzania namna ya kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Lowassa.

Pamoja na hayo, alizungumzia taarifa zilizosambaa nchini, kwamba anamiliki shamba mpakani mwa wilaya za Kongwa na Kiteto ambapo alisema hamiliki shamba lolote katika eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, alimtaka mwenye shida na shamba hilo, akalichukue kama anaamini ni mali yake.

“Wamekuja hapa wanasema mambo ya uongo, nataka niwaambie mambo yafuatayo, kwamba ni uongo kwamba namiliki shamba na namiliki ardhi.

“Mtu ambaye anafikiri ardhi hii ni ya kwangu, kwa ruksa yangu namtaka akachukue bure hilo shamba wanalosema ni la Lowassa, nawaruhusu wakachukue bure.

“Nataka niwahakikishieni sina ardhi huko, na mimi siyo mwendawazimu, kwahiyo anayesambaza uongo huo, akachukue hilo eneo liwe mali yake,” alisisitiza Lowassa.

Wakati Lowassa akiyasema hayo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema Serikali iliyoko madarakani ni dhaifu na kwamba udhaifu huo unachangia uwepo wa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, alisema kama Lowassa angekuwa madarakani, migogoro hiyo inayosababisha mauaji ya wakulima na wafugaji isingetokea kwa sababu ni kiongozi makini na anajua wajibu wake.

“Nawashangaa sana viongozi wetu, yaani watu wanauana mahali halafu waziri mkuu anakwenda kwenye tukio baada ya miezi sita.

“Huu ni udhaifu wa Serikali kwani mimi nilipokuwa waziri mkuu, siku moja watu wawili waliuawa wilayani Kilosa kutokana na mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

“Nilipopata taarifa, nilipanda helkopta mara moja, nikaenda huko na mgogoro huo nikaumaliza, ingawa ulikuja kurudi baada ya kuondoka madarakani.

“Enzi zangu pia kule Ukuryani makabila mawili yalikuwa yakiuana kwa mishale, nikawaambia vijana waandae helkopta niende huko, wakasema nisiende eti kwa sababu wataniua, mimi nilikataa, nikasema nitakwenda huko kwa sababu nyinyi kazi yenu ni kunilinda mimi, na mimi kazi yangu ni kuwalinda wananchi.

“Nilipokwenda huko, mgogoro huo niliumaliza kwa sababu nilikuwa makini tofauti na Serikali yenu ambayo ni dhaifu. Kwahiyo kama Lowassa angekuwa madarakani, nawaambia hiyo migogoro isingekuwapo, mpeni kura awaongoze vizuri,” alisema Sumaye.

Pamoja na hayo, alisema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli haipendi CCM ndiyo maana katika mabango yake anasema ‘Chagua Magufuli’ badala ya ‘Chagua CCM’ kama ilivyozoeleka.

Katika siku ya jana, Lowassa alihutubia mikutano katika majimbo ya Kibakwe, Mtera, Kongwa na Gairo na leo atakuwa mjini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles