25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli ataka stendi Dodoma kuhamishwa

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

Na Pendo Mangala, Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Dodoma kushirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), kuhamisha stendi za mabasi katikati ya mji huo.

Dk. Magufuli amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano katika  Mji wa Dodoma ikiwa ni pamoja na kuutanua ili uweze kukua kwa kasi.

Dk. Magufuli alitoa agizo hilo jana mjini hapa alipokuwa akizindua taa za  kuongozea magari barabarani katika Manispaa ya Dodoma kwenye makutano ya barabara ya Nyerere hadi Mpwapwa, mkoani hapa.

Alisema ni wakati muafaka sasa kwa viongozi wa manispaa na CDA, kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza msongamano katika mji huo ikiwa ni pamoja na kuhamisha stendi hizo za mabasi katikati ya mji.

“Mji wa Dodoma ni mzuri halafu watu wamekuwa wanawekeza kwa kujenga majengo mazuri, hivyo ni vizuri mji huu ukasimamiwa vizuri na manispaa pamoja na CDA, ni vyema ninyi mkaipenda Dodoma kwaniaba ya wananchi wa Dodoma,” alisema, Dk. Magufuli.

Kwa mujibu wa Magufuli siyo miji mingi hapa nchini yenye taa za barabarani na kusisitiza kuwapo kwa taa hizo Dodoma ni muhimu kutokana na kuwa mji mkuu wenye kukua kwa kasi.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Singida, Leonard Kapongo, alisema chimbuko la mradi huo linatokana na kuwapo ongezeko la ajali katika maeneo mengi ya Dodoma.

Kapongo alisema hali hiyo imewafanya kutafuta suluhu ya ajali hizo ikiwa ni pamoja na kuamua kuweka taa za kuongozea magari barabarani.

Alisema mradi huo ulianza kutekelezwa Agosti 20, 2013, chini ya mkandarasi Makenga Investment na kumalizika Mei mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles