25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kikwete awaangukia Watanzania kumuombea Rais Samia

Na Gustafu Haule,Pwani

RAIS mstaafu wa awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kuendelea kumuombea Rais wa awamu ya Sita Dk. Samia Suluhu Hassan ili aweze kutafutia majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi.

Aboubakary Kunenge-Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo  wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu, viongozi wa Serikali, watoto yatima ,wajane na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Pwani katika ifutari iliyoandaliwa Aprili 12, na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge.

Kunenge,ameandaa futari hiyo katika Ikulu ndogo iliyopo Mjini Kibaha kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ambapo mgeni maalum wa hafla hiyo ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Katika hafla hiyo Kikwete,ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuwakumbuka watoto yatima na Wajane kwa kuwapa futari hiyo kwakuwa jamii hiyo inapaswa kutunzwa na watu wote.

Amesema kuwa,kitendo cha kuandaa futari hiyo ni kumtukuza Mungu hasa katika kuwasaidia yatima ambao mahitaji yao yanategemea misaada ya wahisani mbalimbali.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa moyo wake na tuendelee kumuombea ili hapate afya njema na umri mrefu ili haweze kuongoza zaidi Taifa letu kwa kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili Watanzania,”amesema Dk Kikwete

Kikwete amepongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge kwa kazi nzuri anayofanya ndani ya Mkoa kwakuwa amekuwa kiongozi anayejali maendeleo ya Mkoa kiuchumi.

Kwa upande wake mkuu wa Pwani Abubakari Kunenge,amesema kuwa ameandaa futari hiyo kwa niaba ya Rais Samia na lengo kubwa ni kuwakutanisha yatima na Wajane.

Kunenge, amesema kuwa hatahivyo jumla ya yatima 150 na Wajane 50 wameshiriki futari hiyo na shukrani nyingi zimuendee Rais Samia kwakuwa ndiye aliyeandaa futari hiyo.

Aidha Kunenge ametumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi kuhakikisha wanawatunza watoto wao katika maadili yanayofaa ili wasijiingize katika vitendo vilivyo kinyume na utamaduni wa Tanzania .

“Wazazi tunzeni watoto wenu wasiingie katika vitendo viovu ,tuwalee vizuri ,nasema hivyo kwasababu sasa hivi nchi yetu imeingia katika janga, hivyo lazima tufuate maadili yetu na kila mtu atekeleze wajibu wake,”amesema Kunenge.

 Kunenge ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kufanya shughuli za kilimo ili wajiongezee kipato na kwa watumishi wa Serikali ataka waache ufisadi na wafanyekazi kwa uadilifu.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani Hamis Mtupa ,amewaonya wale wanaoandika miradi kwa ajili ya kuomba fedha kwa ajili ya watoto yatima kuacha kutumia kichaka hicho kwa ajili ya maslahi yao.

Mtupa,amesema wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia watoto yatima kama mtaji wa maisha yao na kwamba wanapopata fedha hizo utekelezaji watoto hao na hatimaye kuangalia maslahi yao jambo ambalo halimpendezi Mungu.

Hata hivyo, Mtupa aliongoza dua maalum ya kumuombea Rais Samia ili aweze kutimiza majukumu yao vyema ikiwa ni sehemu ya kumpa moyo wa kuendelea kusaidia yatima,Wajane na hata wenye mahitaji maalum.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles