NA AMINA OMARI, TANGA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, ameziagiza halmashauri zote nchini kusimamia sheria ndogo ndogo za kudhibiti tabia ya watu kuivisha matunda kwa kutumia moto.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said kwa niaba ya Dk. Kigoda, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kutokomeza inzi wanaoshambulia matunda mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Dk. Kigoda, uuzwaji wa matunda yaliyoivishwa kwa njia ya moto unamsababishia mkulima hasara badala ya kumuongezea faida.
“Ni vema sasa halmashauri zikasimamia sheria ndogondogo ili kudhibiti uharibifu huo wa matunda kwa kuhakikisha matunda hayo yanauzwa yakiwa yamekomaa tayari.
“Pamoja na hayo, hata maofisa ugani wanatakiwa kuendelea kutoa elimu juu ya usafi wa mashamba ili kuweza kupunguza wingi wa inzi waharibifu wa matunda.