33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kamani atakiwa kuacha kulalamika

Mbunge wa Jimbo la Busega,Mh. Titus Kamani
Mbunge wa Jimbo la Busega,Mh. Titus Kamani

NA MWANDISHI WETU, BUSEGA

MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Busega, Simiyu, Mshoni Mshoni, amemtaka Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Titus Kamani, kuacha kutumia vyombo vya habari kupotosha wananchi, badala yake awapelekee maendeleo huku akitekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Mshoni alisema tabia ya mbunge huyo kutumia vyombo vya habari kupotosha ukweli wa hali halisi ilivyo jimboni inawachanganya wanachama na wananchi.

Mwenyekiti huyo alisema hayo baada ya kuwapo taarifa za upotoshaji zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari siku kadhaa, zikielezea malalamiko ya mbunge huyo akidai anachafuliwa na kuhujumiwa na makundi ndani ya chama katika kutekeleza majukumu jimboni kwake.

Mshoni alisema upotoshaji huo unawachanganya kisiasa wanaCCM na wananchi na kusababisha ziundwe tume mbili, kutafuta ukweli na kujiridhisha kuhusu malalamiko ya mbunge huyo dhidi ya chama chake, wanachama na wananchi, akidai anachafuliwa na kuhujumiwa na makundi ndani ya chama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

“Tume ya kwanza iliundwa mwaka 2012, iliongozwa na Katibu wa Uenezi Mkoa wa Mwanza, Simon Mangerepa, tume ya pili iliundwa tena Januari mwaka huu, ikiongozwa na Katibu wa Maadili, Alhad Mbengula. Hizi tume zote hazikubaini sehemu ambayo mbunge anahujumiwa.

“Mimi kama Mwenyekiti wa chama wilaya, viongozi na wanachama wa CCM, tunasikitishwa na tabia hii ambayo haikubaliki kwa viongozi, na hasa chama chetu.

“Tumemwita mbunge kwenye vikao vingi vya chama, lakini hafiki. Tunaamini angekuwa anafika basi hoja zake angezitoa ili kama kuna tatizo litatuliwe na si kila kukicha tunasoma kwenye magazeti malalamiko yake tu,” alisema Mshoni.

Alisema kinachofanywa na mbunge huyo ni kinyume na misingi na maadili ya CCM.

“Tutamwita kwenye vikao vya chama ili athibitishe tuhuma hizi dhidi ya wanachama wanaomhujumu. Vinginevyo akishindwa atachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kumpeleka mbele ya Kamati ya Maadili. Hatupendi viongozi wasiotimiza wajibu na kazi yao inakuwa kulalamika na kubaki kulaumu wengine,” alisema Mshoni.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Wilaya ya Busega, Samwel Ngofilo, alikana madai ya vijana kutumiwa kumhujumu mbunge huyo.

Alisema hali hiyo ni dalili ya woga kwa sababu ya kutoonekana jimboni mwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles