Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani, amesema Tanzania inashika nafasi ya kwanza Afrika katika kuunganisha umeme vijijini ikiwa imefikia asilimia 74 ya vijiji vyote.
Alisema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.
“Awali, Nigeria ndiyo ilikuwa ikiongoza ikiwa na asilimia 72 lakini tumeipita, tukiwa tumefikia zaidi ya asilimia 74 na hivyo tunaongoza Afrika kwa sasa,” amesema Waziri.
Dk Kalemani alisema vijiji 9,001 nchini vimeshaunganishiwa umeme na kwamba na kati ya hivyo, 3,559 vimeunganishiwa umeme kupitia Mzunguko wa kwanza wa Awamu ya Tatu ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA III-1), unaoendelea hivi sasa.
Alisema mradi wa REA III-1 utakamilika Juni lakini Serikali imekubaliana na wakandarasi wote wanaotekeleza mradi huo nchi nzima, kukamilisha kazi husika miezi miwili kabla, hivyo wanatarajiwa kukabidhi kazi kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ifikapo Aprili 31.
Kwa upande wa Wilaya ya Masasi, Dk Kalemani alisema Serikali iliamua kurejea mpango-kazi na kufanya mabadiliko ambayo yaliwezesha kuongeza idadi ya vijiji vitakavyonufaika na mradi huo wilayani humo.
“Katika mpango wa awali ni vijiji vichache tu vya Masasi ndivyo vilikuwa vinufaike na mradi huu. Hii ni kwa sababu vijiji vingine viko katika halmashauri za miji na siyo wilaya hivyo vilikuwa vinakosa sifa kwani vilikuwa na hadhi ya mitaa na siyo vijiji.”
Akijibu hoja za wananchi wa vijiji vya Namikunda A na B, Nagaga na Matogolo kuhusu changamoto ya umeme kukatika mara kwa mara, alisema tayari Serikali imeshughulikia tatizo hilo kwa kuunganisha baadhi ya maeneo ya Mtwara katika gridi ya taifa.
Aliyataja maene hayo kuwa ni Tunduru, Masasi na Nanyumbu na kwamba yameunganishwa kupitia mradi wa umeme mkubwa wa Makambako – Songea (kilovoti 220).
Katika ziara hiyo ambayo Waziri aliviwashia umeme vijiji vya Nagaga na Matogolo, ametoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia ili waunganishiwe umeme.
Aliwataka wananchi kutumia simu zao za mkononi kuwapiga picha na kuwarekodi mameneja wanaogoma kupokea malipo husika wakati umeme umeshafika kwenye maeneo yao na kuziwasilisha wizarani kama ushahidi ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.
“Kamwe hatutawavumilia mameneja wa aina hiyo kwa sababu siyo tu wanalikosesha shirika mapato lakini pia wanaichonganisha serikali na wananchi kwa kuchelewa kuwapatia huduma husika,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Dk Kalemani aliwasihi wananchi kuwa wavumilivu pale inapotokea huduma ya umeme imekatwa hususani katika kipindi cha mvua huku akieleza kuwa hali hiyo inasababishwa na kufanya ukarabati wa miundombinu ambayo imekuwa ikiathiriwa na mvua.
Aliwataka ka watendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuhakikisha wanatoa taarifa kwa wananchi pindi wanapolazimika kukata umeme ikiwa ni pamoja na kufanya matengenezo kwa muda mfupi ili kurejesha huduma.