28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Madiwani Ilemela wadai kuhatarishiwa nafasi zao

NA BENJAMIN MASESE

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamegeuka ‘mbogo’ dhidi  watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)  na  Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura), wakiwatuhumu kuwahujumu na kuwahatarishia nafasi zao kuelekea uchaguzi ujao wa Oktoba.

Wakiongozwa na Mbunge wao, Angelina Mabula ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, walisema hivi sasa hali zao si nzuri ndani ya kata zao kutokana na wananchi kuwadai huduma za umeme na maji kwa muda mrefu.

Wamesema kuwa wamekuwa wakiwapa wananchi ahadi za matumaini ambazo zimeshindwa kutekelezwa kwa wakati, hivyo walipendekeza kujigeuza kuwa kamati ili kuwachukulia hatua kabla ya kuadhibiwa na sanduku la kura.

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ilemela, John Wanga aliingilia kati mpango wa madiwani hao  kujigeuza kuwa kamati na kuwaeleza kwamba watumishi wa Mwauwasa na Tarura  hawawezi kuadhibiwa na madiwani isipokuwa wana mamlaka za uteuzi wa nafasi zao.

Wanga aliwaeleza madiwani hao kwamba kama wanaona watendaji wa Mwauwasa na Tarura hawatimizi wajibu wao ipasavyo, basi taarifa zitafikishwa kwa mamlaka zao za uteuzi kupitia vikao vya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

Hayo yalijiri juzi katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichokutana kujadili taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya robo ya pili ya mwaka 2019/2020 ambapo walianza na kipindi cha dakika 30 za maswali matano na majibu ambapo wote walielekeza kero zao kwenye maji, barabara na umeme.

Maneja wa Tanesco Wilaya ya Ilemela, Fidelis Chaula alisema tatizo linalowakabili na kushindwa kufikisha umeme maeneo yote ya kata na mitaa, ni kuadimika kwa waya  kutokana na uzalishaji kuwa  mdogo kuliko mahitaji yaliyopo nchini, huku akiwaahidi madiwani hao kwamba kufikia Juni  huduma hiyo itakuwa imewafikia wananchi wote.

Naye mhandisi wa Mwauwasa, Selestine Mahubi, alisema tatizo la maji ndani ya Ilemela na Nyamagana litakwisha  muda si mrefu baada ya kumalizia ujenzi na  uunganishaji mabomba katika matanki ya Nyasaka, Kitangiri, Mji Mwema, Igongwa na Nyamhongolo.

Mahubi aliwataka madiwani hao kutohofia nafasi zao kwani huduma hiyo baadhi ya maeneo imeanza kuonyesha matumaini ya kudumu.

Kwa upande wa Mhandisi wa Tarura Wilaya ya Ilemela, David  Christopher ambaye muda wote alikuwa akisaidiwa kujibu maswali na maofisa wenzake, wakiwamo Nelson Mfinaga na Goefrey Mamkwe, alisema utekelezaji wa miradi ya barabara inategemea na bajeti iliyopo na pesa zilizotolewa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles