28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Ndugulile akagua utayari kutibu corona Kilimanjaro

Na Safina Sarwatt

WATUMISHI  wa Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuwa na utayari wa dawa na vifaa tiba katika jengo maalumu la maradhi ya mlipuko, ili liweze kutoa huduma stahiki kama atatokea mgonjwa mwenye  virusi vya corona. 

Kauli hiyo ilitolewa na  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati alipokagua jengo maalumu la maradhi ya mlipuko na kuzungumza na baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo.

 Alisema tayari serikali imeshakamilisha kila kitu kinachohitajika hivyo hawana budi kujipanga ili kutoa huduma stahiki endapo atapatikana mtu mwenye virusi hivyo kwenye eneo hilo. 

Dk Ndungulile alisema hadi hivi sasa hakuna kisa cha mtu yoyote nchini mwenye virusi hivyo lakini Serikali inajipanga kuhakikisha itakabiliana navyo endapo vitafika nchini.

“Kwakuwa jengo hilo ni la dharura hata watumishi watakao toa huduma wanatakiwa kukaa mkao wa dharura wakati wote kwasababu ugonjwa hauna muda maalumu, ifahamike kwamba dereva wa gari la wagonjwa ni nani, anayesimamia utunzaji dawa ni nani, gari ipi itakayo tumika ili kuondoa sitofahamu pindi itakapotokea, “alisema.

Dk Ndungulile alisema haitakuwa vyema Serikali kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya kutoa huduma za magonjwa ya dharura na mgonjwa akitokea ashindwe kutibiwa.

Tume ya Afya ya China jana ilisema kulikuwa vifo vipya 143, hivyo idadi ya waliofariki dunia kutokana na virusi hivyo mpaka sasa ni 1,523. Kati ya vifo hivyo vipya, vinne viliripotiwa katika mji wa Hubei.

Pia watu wengine 2,641 wamethibitishwa kuwa na virusi hivyo na kufanya idadi ya waathirika wa janga hilo mpaka sasa kufikia 66,492.

Mbali hayo pia aliipongeza  hospitali hiyo kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa Serikali wa GEPG kutoka sh millioni 1 hadi milioni 8 kwa siku.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mawenzi, Dk. Jumanne Karia alisema hivi sasa wanajipanga na timu yake katika kuhakikisha huduma bora za matibabu zinatolewa sambamba na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

“Hospitali imejipanga kuhakikisha inaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza ukusanyaji wa mapato, ambapo kwasasa hospitali kwa siku inakusanya milioni 8 na bima ya afya milion 180 kwa mwezi, “alisema. 

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles