28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Chami:Nilikosa kuungwa mkono jimboni

chamiNa RAMADHAN HASSAN

Dk. Cyril Chami ni miongoni mwa vigogo wa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioangushwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Dk. Chami, ambaye ni mwalimu kitaaluma, alipata kuongoza Jimbo la Moshi Vijijini kwa vipindi viwili katika utawala wa awamu ya nne.

Pia aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Akiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alisimamia maamuzi yake, pale ilipotakiwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege ajiuzulu, kwa kile kilichodaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyokuwa ikikagua magari yaliyokuwa yanatoka nje.

MTANZANIA limefanya mahojiano ya ana kwa ana mwanasiasa huyo, ambaye kwa sasa amerudi kufundisha baada ya kushindwa ubunge katika uchaguzi wa mwaka jana.

Pamoja na mambo mengine, anazungumzia namna alivyoshindwa na Antony Komu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Endelea…

MTANZANIA: Ulipata kushika nyadhifa mbalimbali katika utawala wa Jakaya Kikwete, ni jambo gani ambalo unalikumbuka?

  1. CHAMI: Nakumbuka ustahimilivu, busara, hekima pamoja na kuishi vizuri na watu, ilifikia kipindi mpaka unaogopa unasema tutavuka salama kweli, lakini jamaa alikuwa na busara za ajabu.

Akiona mambo yamebadilika anaahirisha kikao, baadaye mnarudi tena hasira zinakuwa zimepungua, mambo yanaendelea na mnatoka salama.

Pili, nakumbuka kuhusiana na masuala ya diplomasia katika kipindi cha JK, nchi imejipatia marafiki wengi.

Tatu, uchumi wetu ulikuwa unacheza kwenye asilimia saba hata kama kulikuwa na wapigaji, lakini uchumi ulikuwa upo vizuri.

Nne, demokrasia ilipanuka mno, kila mtu alikuwa anaongea, wengine walifikia mpaka wakawa wanamtukana Rais, lakini alikuwa hawajibu.

MTANZANIA: Unaionaje demokrasia ya sasa na enzi za JK?

  1. CHAMI: Sasa hivi jamaa ni mkali na mimi nasema Magufuli yupo sahihi, haiwezekani kila mmoja ahubiri siasa tu, kila mtu afanye katika jimbo lake na Rais angurume popote, si ndio mwenye nchi.

Nashauri Rais avifute vyama ambavyo havina uwakilishi katika udiwani wala ubunge kutokana na kujaza idadi tu, hata Marekani na Uingereza kuna vyama vichache tofauti na Tanzania.

Haya yote yamesababishwa na huruma ya JK, lakini hivi vyama vidogo vinatakiwa viungane ili viwe chama kimoja.

Pia hata CCM wangeungana tu na Tanzania Labor Party (TLP) ili kiwe chama kimoja.

MTANZANIA: Unasema TLP kingeungana na CCM?

  1. CHAMI: Ndiyo, kwa sababu TLP ni chama kidogo, hivyo lazima kiungane na kikubwa, lakini pia Augustine Mrema amekuwa karibu na CCM.

MTANZANIA: Unauonaje utawala wa Rais Magufuli?

  1. CHAMI: Unakwenda vizuri, udhibiti wa mapato umeongezeka, mianya ya kupata fedha bila kujishughulisha imezibwa na kama tunavyojua, ile methali yetu asiyefanya kazi na asile, hivyo kwa Magufuli usipofanya kazi huli.

Mtu yeyote anayetaka maendeleo ya nchi hawezi kupingana na Rais Magufuli, ila wale wa Mission Town, wakwepa kodi na wajanja wajanja ni lazima wamchukie.

Mfano unakuta Mkurugenzi anachaguliwa, ndani ya muda mfupi ana hoteli ya nyota tano, fedha kapata wapi, hivi huyu ambaye anafanya kazi kwa moyo mmoja atajituma kweli, si atakuwa anawaza wizi tu.

MTANZANIA: Unamshauri nini Rais Magufuli?

  1. CHAMI: Awekeze kwa kujenga viwanda kwa fedha za serikali kama alivyofanya kwa kununua ndege kwa fedha za serikali, kwa kufanya hivyo ataitoa nchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Lakini ni lazima atafute menejimenti ya kuviendesha viwanda hivyo, kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa katika mikono salama, kwani kutakuwa na ajira ambazo zitatolewa na viwanda hivyo.

Hapa nasisitiza, ila najua nitapingana na wachumi wenzangu, Magufuli ajenge viwanda kwa fedha za serikali kwa usalama wa nchi, kwani vijana wengi watakuwa na ajira.

MTANZANIA: Unaposema ajira zinalinda usalama wa nchi unamaanisha nini?

  1. CHAMI: Ajira ni kigezo muhimu cha kulinda usalama wa nchi, tukiwa na viwanda huwezi kusikia mambo ya ajabu ajabu, jambo la msingi serikali ijenge viwanda.

MTANZANIA: Wakati ukiwa Waziri wa Viwanda na Biashara ni jambo gani ambalo umelianzisha na linaendelea kuwepo hadi leo?

  1. CHAMI: Bar Codes ni jambo ambalo nililianzisha mimi na linaendelea hadi leo kuwepo katika vifungashio na limekuwa likinufaisha wengi.

Pia kulikuwa na trekta la kwanza lililotengenezwa Tanzania.

MTANZANIA: Ni sekeseke gani ambalo hutalisahau wakati ukiwa Waziri wa Viwanda na Biashara?

  1. CHAMI: Ni mradi wa Mchuchuma na Liganga, wakati tunasaini mkataba huo ‘interest’ zilikuwa nyingi, ilifikia wakati mkataba ulitekwa nyara na viongozi fulani, ila tulipotishia tunakwenda kwa rais mkataba ulirudishwa.

Pia bodi ya NDS ilitishia kujiuzulu chini ya Mwenyekiti Christant Mzindakaya, kutokana na jambo hilo.

MTANZANIA: Wakati ukiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ulijifunza nini?

  1. CHAMI: Ilikuwa mwaka 2006 mpaka 2008, nimejifunza mambo mengi sana, hasa katika suala la Economic Diplomatic, ukiona vyaelea ujue vimeundwa, nimehusika katika nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje katika suala la Diplomatic.

Ila naomba nitoe ushauri, kwanini Wizara za Mambo ya Nje na Viwanda, Biashara na Uwekezaji zisiwekwe pamoja, mimi naona asilimia 75 ya mambo ambayo yapo Wizara ya Mambo ya Nje inazungumzia biashara.

MTANZANIA: Unauzungumziaje ugomvi wako na aliyekuwa Naibu Waziri wako, Lazaro Nyalandu?

  1. CHAMI: Hivi yule Charles Ekelege si alikuwa mteule wa Rais, hivi nani anaweza kutengua uteuzi wa Rais, wanaofanya hivyo hawajui majukumu yao, mimi nilikuwa najua majukumu yangu, nisingeweza kumfukuza.

Mpaka sasa waliokuwa wakidai ni kosa kwa Ekelege la kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni iliyokuwa inakagua magari yaliyokuwa yanakuja Tanzania hakuna aliyethibitisha, si kamati ya kina marehemu Deo Filikunjombe na Kangi Lugola, wala Mahakama.

Ukweli unabaki pale pale, mimi sijihesabii kuwa mkosaji katika hilo kwa kutomhukumu ambaye hakuwa na kosa, sijaona kama nina kosa, hakuna ushahidi katika hilo na mimi dini yangu hairuhusu kumwonea mtu.

Kila mmoja anajua kuwa mwenye uwezo wa kutengua uteuzi wa Rais ni Rais mwenyewe, sasa pamoja na mashinikizo ya nimtimue kazi lakini mimi nilikataa sababu hakukuwa na ushahidi, pamoja na kuwa ni mteule wa Rais, kama niliwajibishwa kwa jambo hilo mimi hadi leo nafsi yangu ipo ‘clear’.

MTANZANIA: Ilikuwaje ukaanguka ubunge?

  1. CHAMI: Wimbi la Edward Lowassa kwenda upinzani ndiyo sababu kubwa ya mimi kuanguka katika jimbo langu kule Arusha, Manyara na Kilimanjaro walijua mkombozi wao ni Lowassa.

Wananchi walijua rais atakuwa Lowassa, hivyo na upande wa wabunge wale waliokwenda kupiga kura wote walikuwa wanapiga kwa Lowassa na kwa wabunge walikuwa wanachagua wa Chadema ndiyo maana unaona katika mikoa hiyo mitatu niliyokutajia yote imechukuliwa na Chadema.

Ila nilifanya kampeni katika wakati mgumu kutokana na watu wote kumtaka Lowassa na Chadema, nilipambana na nilikuja kushindwa dakika za mwisho na Antony Komu.

MTANZANIA: Unaonaje kasi ya kuwaletea maendeleo aliyonayo Mbunge wa sasa katika Jimbo la Moshi Vijijini?

  1. CHAMI: Hili nawaachia wapiga kura wangu waangalie, wakati nikiwa mbunge na huyo wa sasa je, katika suala la maendeleo itakuwaje ili mwaka 2020 sasa waje wafanye maamuzi sahihi?

Katika jimbo langu suala la elimu nililiacha vizuri, kwani katika kata 29 kuna shule 16 za kidato cha tano na sita, sasa tulikuwa tunakwenda katika ujenzi wa mabweni.

Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru wale walionipigia kura, ninajivunia nimewafanyia mambo mengi ambayo ninajivunia, tutakutana 2020 Mungu akitupa uzima.

Sababu nyingine iliyofanya nipoteze ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini ni katika jimbo lile kulikuwa na viongozi wa vyama vingine  ambao ni James Mbatia wa NCCR Mageuzi, Agustino Mrema, Philemon Ndesamburo na Edwin Mtei.

Hawa wote ni viongozi wakubwa katika vyama vyao na wengine ni waanzilishi wa vyama hapa nchini, wote wanatoka katika jimbo langu, sasa hawa wana watu wao ambao inakuwa rahisi kushawishi wasinipigie kura.

MTANZANIA: Je, Serikali imechelewa au imewahi kuhamia Dodoma?

  1. CHAMI: Tumechelewa, tulipaswa kufanya mapema, Dar es Salaam kumejaa, inaumiza unatoka nyumbani wakati mwingine unatumia zaidi ya masaa matano njiani.

Makao Makuu kuja Dodoma huo ni  mgawanyo mzuri wa keki ya Taifa, Magufuli amefanya sahihi kabisa serikali kuhamia Dodoma.

MTANZANIA: Hivi sasa unajishughulisha na nini?

  1. CHAMI: (Anacheka) mimi ni mwalimu, nimerudia kazi yangu, sasa hivi ni mwalimu katika Chuo Kikuu cha St John cha mkoani Dodoma, nafundisha uchumi.

MTANZANIA: Unaionaje CCM ya sasa?

  1. CHAMI: CCM imezidi kuwa nzuri, hakuna chama kitakachoweza kuifikia CCM, kwanza kuna demokrasia, lakini ndio chama pekee wanachama wana sauti kuliko vyama vyote.

Hivyo kwenye nafasi ya urais bado wapinzani wataendelea kusubiri sana, kutokana na Rais Magufuli kukubalika kwa wananchi.

MTANZANIA: Unaonaje kuhusiana na Rais kuwapa madaraka vijana?

  1. CHAMI: Rais yeyote ana utashi wake, ila sisi ni wajibu wetu kumuunga mkono bila kuangalia anaowapa nafasi kama ni vijana au ni wazee.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles