30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Angela Merkel anapovalia njuga ngoma anayocheza

angela-merkelWASWAHILI husema kuwa; ‘Ukitaka kujua uhondo wa ngoma uingie ucheze’ usibaki kuitazama tu kwani hutajua siri ya njuga zinazohanikiza mirindimo yake, ndivyo unavyoweza kumlinganisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliyeicheza ngoma ya uhamiaji pembeni na kuhatarisha nafasi yake kisiasa kwa kuwakaribisha wahamiaji lukuki nchini mwake bila kujali hasira za wananchi wake.

Sasa ameamua kuvalia njuga ngoma hiyo na kuingia dimbani kutokana na ziara yake aliyoifanya hivi karibuni barani Afrika, ingawa aliyoyaahidi ziarani mwake yanaweza kuwatibua zaidi wananchi wa Ujerumani.

 Mwezi mmoja na nusu uliopita niliwahi kuandika kuhusu Kansela huyo mwanamama mwenye uhafidhina wa msimamo wa shingo ngumu katika medani ya siasa za taifa lake, alipogalagazwa kwenye uchaguzi kwa chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) kupigwa kumbo na chama cha Alternative fuer Deutshland (AfD) chenye uhafidhina mkali dhidi ya uhamiaji katika jimbo la Mecklenburg Pomerania, ambapo CDU kilishika nafasi ya tatu nyuma ya chama cha SPD na cha wahafidhina kilichoshika nafasi ya pili.

Hiyo iliashiria kupingwa kwa Kansela Merkel kwa ukarimu wake uliopitiliza kwa wahamiaji akipingana hata na viongozi wenzake wa Ulaya (EU).

AfD kimetumika kuashiria mweleka wa CDU katika uchaguzi ujao wa Bunge la nchi hiyo mwakani, kwa kuwa ushindi wa SPU na AfD umekichoma mkuki moyoni chama cha CDU kama chenyewe kilivyokiri na kiliahidi kujipanga upya lakini inavyoelekea kujipanga kwake ni kwa kinara wake Merkel kujiimarisha kwenye msimamo wake wa uhafidhina wa ukarimu kwa wahamiaji.

Kansela Merkel alipoanza ziara yake barani Afrika alipofika nchini Niger aliahidi kuwa nchi yake itatoa msaada wenye thamani ya Euro milioni 27 ili kuwezesha kupambana na ugaidi na kuzuia wahamiaji kuingia Ulaya.

 Niger imekuwa kipito kinachotumiwa na wahamiaji kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaovuka Bahari ya Mediterranean kuingia Ulaya.

Katika msaada huo Euro milioni 10 zitatengwa kwa ajili ya ununuzi wa zana za jeshi la nchi hiyo na nyingine Euro milioni 17, kulisaidia eneo la kitalii la Agadez ambalo limekumbwa na kadhia ya kutumika kama njia ya kusafirishia wahamiaji haramu, lakini pia likidhoofika kiuchumi kutokana na kudorora kwa biashara ya utalii kulikosababishwa na mashambulizi ya ‘Kijihadi’ na utekwaji nyara watalii.

Takriban watu 12,000 wakiwamo wanawake na watoto hukimbia Agadez kila wiki na kujitosa kwenye safari ya hatari wakipitia jangwani kuelekea Libya, wanakosombwa na mashua zisizo salama wengi wao wakiona heri kufia baharini kwa kuzama kuliko kubaki eneo hilo ambalo ni kiini cha wahamiaji kutoka Niger.

Lakini usidhani Wajerumani wanaopingana na kiongozi wao juu ya wahamiaji watafurahia msaada huo ili kupunguza ujio wa wahamiaji nchini mwao, kwani fedha hizo zitakazotolewa msaada zinatokana na mapato ya nchi yao zikiwamo kodi zao zilizokusanywa.

Kabla ya Niger, Merkel alianzia nchini Mali alikojikita zaidi katika kuhakikisha usalama kwa kusaidia kuimarisha jeshi, kwa kuwa vurumai za mapigano zinasababisha wataalamu wengi barani Afrika kutotumikia nchi zao kwa kukimbilia Ulaya.

8Hiyo maana yake ni kwamba ukuaji wa uchumi wa nchi hizo utadorora kwa kukosa wataalamu wenye mchango muhimu na umasikini utakaojiri, utasukumia wimbi zaidi la wahamiaji watakaokimbilia Ulaya mtazamo uliokubaliwa na mwenyeji wake Rais Boubacar Keita ambaye mamia ya vijana kutoka nchini mwake wameangamia katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kufika Ulaya.

Mama yetu Merkel anayewapenda sana wahamiaji kiasi cha kupingana na wananchi wake akatua Ethiopia alikokuwa na ajenda tofauti kidogo, inayohusiana na vurumai za kisiasa ambapo hivi karibuni watu 50 wameuawa katika maandamano ya kupinga mbinyo wa Serikali wakati hali ya hatari ikitangazwa nchini humo lakini takriban watu 400 wameuawa ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Hakuna shaka kuwa Ethiopia nayo ikiendelea hivyo wahamiaji wataanza kutafuta njia ya kwenda Ulaya kukimbia madhila hayo, lakini Kansela Merkel amebainisha kuwa lazima Ulaya ibadilishe mtazamo wake kuhusiana na suala la wahamiaji kutoka barani Afrika, kwamba ustawi wa Bara hili ni kwa mustakabali wa Ujerumani na Ulaya yote na haiwezekani kubadili hali mara moja lakini pia haiwezekani kuangalia tu wakati wengine wakiangamia kwani si suala la kuoneana huruma bali thamani ya utu wa binadamu inayonadiwa na EU.

Kwa kuwa hata juhudi za kufunga vipito vingine vya wahamiaji haramu hazijatatua hali hiyo kwani bado kuna changamoto kama hizo Uturuki, Ugiriki na kwingineko na haiwezekani kukodolea macho wakati hatari dhidi ya uhai ikiongezeka nchini Iraq na Syria na matatizo hayo hayataisha kwa kuyapuuza.

Usalama na amani ya Ujerumani inahusisha maisha ya watu wengine pia hata kama wako mbali na kama ustawi unaotakiwa ni kuwajali Wajerumani pekee bila wengine, basi hiyo ni ndoto isiyowezekana na hivyo ndivyo anavyoamini Merkel ingawa Wajerumani wenzake wamemgeuka kimtazamo kutokana na kuhisi wimbi kubwa la uhamiaji linawaathiri kiuchumi. Jibu la nani yuko sahihi baina ya Kansela na wananchi anaowaongoza litajulikana kwenye uchaguzi wa mwakani nchini humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles