FRANCIS GODWIN Na RAYMOND MINJA-IRINGA
KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amemkaribisha Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ajiunge na chama hicho.
Amesema hiyo ni kwa sababu Zitto ni miongoni mwa wanasiasa wanaojua kujenga hoja za uchumi.
Pamoja na kutoa mwaliko huo, Dk. Bashiru alishangazwa na ukimya wa Zitto kuhusu suala la korosho kama alivyokuwa akijenga hoja kuhusu suala la mgodi wa Buzwagi uliopo mkoani Shinyanga.
Kauli hiyo aliitoa Iringa jana alipozungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.
Alisema Zitto ni kijana mwenye uwezo wa kupambanua mambo ya uchumi kwa sababu hata wakati wa suala la Buzwagi alionyesha uwezo mkubwa wa kupambanua mambo.
“Hakuna kijana mzuri mwenye uwezo wa kupambanua mambo ya uchumi nchini kama Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe.
“Wakati wa suala la Buzwagi yeye ndiye aliweza kuonyesha uwezo mkubwa wa kupambanua mambo kwa vile hata mikutano yake ilikuwa na mwitikio mkubwa kutokana na umaarufu alioupata kwa hoja zake nzito za kujenga hoja bungeni.
“Ila leo wakulima wa korosho nchini walikuwa wakiminywa Zitto yupo kimya… nasema Zitto ni kijana mzuri ila chama alichopo si cha kijamaa kama CCM ni vizuri aje CCM kuungana na chama cha kijamaa kinachopinga unyonyaji,” alisema Dk. Bashiru.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa CCM alishangazwa na ukimya wa viongozi wa vyama vya siasa wakati wa suala la korosho mikoa ya kusini.
“Uchunguzi umeonyesha wakulima walikuwa wakinyonywa na viongozi wa vyama vya siasa wakiwamo baadhi kutoka ndani ya CCM kama wabunge, mawaziri na ndiyo sababu wengi walichukizwa na serikali ya Rais Dk. Magufuli, kuchukua uamuzi wa kununua korosho hizo ila sisi kama chama tunapongeza hatua hii amhayo sasa imekwenda kinyume na matakwa ya wanyonyaji wachache,” alisema
WALIOFUKUZWA
Dk. Bashiru alitoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM ambao walikuwa wanatumikia adhabu ikiwamo kufukuzwa unachama na kuvuliwa nafasi za uongozi kutokana na kujenga makundi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kuandika baru za kuomba msamaha na watasamehewa.
“Nataka kutumia hadhara hii kuwataka wale ambao walisimamishwa, kuvulia uongozi na hata uanachama ndani ya chama chetu kuandika barua za kuomba msamaha tutawasamehe maana chama hiki ni chetu sote.
“Tunatambua kutokana na yule waliyemtegemea kuondolewa kugombea nafasi ya urais mwaka 2015 wengi walisaliti chama chetu na vikao vya juu vilifanya uamuzi wake ila wanaweza kuandika barua kuomba kusamehewa tutawasamehe,” alisema Dk. Bashiru.
Pamoja na hali hiyo aliwataka wanachama wa CCM kuendelea kuheshimu maadili ya chama hicho na maagizo mbalimbali yaliyotolewa na chama.
Alisema hakutakuwa na msalie Mtume mwana CCM ambaye ameanza mchakatoi wa kujinga kwa ajili ya udiwani, ubunge ama urais.
Vilevile alishangazwa na kuibuka vurugu za kusaka urais wa Zanzibar mwaka 2020 kwa baadhi ya wana CCM kuanza kujenga makundi jambo ambalo ni kinyume na kanuni na katiba ya chama hicho tawala.
Alisema CCM ni chama kinachoendeshwa kwa misingi na si chama ambacho kiongozi wake anatokana na kuomba kuchaguliwa bali hupatikana kwa utaratubu na si kujipitisha ama kugawa pikipiki, baiskeli au zawadi mbalimbali.
kusema ukweli ni vizuri,na mpe sifa mtu kwa kile anacho sitaili na muelimishe ili ajitabue.