Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KOCHA Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amepingana na mashabiki wa soka wanaoponda kiwango cha mahasimu wao Yanga, kwa kusema vigogo hao wa Jangwani bado wana kikosi cha ushindani.
Simba juzi ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao la Simba katika mchezo huo lilifungwa na beki, Erasto Nyoni, baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya kiungo, Shiza Kichuya.
Licha ya kupata ushindi, kikosi cha Simba pia kilionekana kutawala asilimia kubwa ya umiliki wa mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki lukuki.
Akizungumza na MTANZANIA, Djuma, alisema pamoja na ushindi walioupata kwenye mchezo huo ni makosa kuponda ubora wa kikosi cha wapinzani wao Yanga.
“Binafsi bado naamini Yanga ina kikosi kizuri ndiyo maana unaona tumepata ushindi, lakini haikuwa kazi rahisi, ilitubidi kupambana kweli kweli ili kupata matokeo
“Mimi nakwambia hata huko kwenye mashindano ya kimataifa inaweza kufanya vizuri zaidi na sitashangaa hilo kama litatokea, kwa hiyo ni makosa kusema timu rahisi,” alisema Djuma na kuongeza:
“Wanachotakiwa ni kufanya maandalizi ya uhakika tu kwa kuwa hakuna kitu kingine cha ajabu ambacho wanachokihitaji.”